LIVE STREAM ADS

Header Ads

Uzinduzi wa zoezi la upuliziaji viua dudu kwenye mazalia ya mbu

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Mohammed Kahundi amezindua zoezi la Upuliziaji wa Viua Dudu ‘Larviciding’ katika mazalia ya mbu mkoa wa Shinyanga ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kupambana na ugonjwa wa malaria nchini ili kutekeleza kauli mbiu ya ‘Ziro Malaria inaanza na mimi’. 

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumamosi Desemba 21,2019 katika bwawa la Shunu lililopo katika halmashauri ya Mji Kahama na kuhudhuriwa na Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya,wajumbe wa timu ya usimamizi za afya mkoa na halmashauri,wadau wa maendeleo asasi ya T- MARC Tanzania na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Upuliziaji wa Viua Dudu katika mazalia ya mbu ulioongozwa na kauli mbiu ya 'Ziro Malaria inaanza na mimi' Kahundi alisema Viuadudu vinavyotumika kuweka katika madimbwi ya maji havina madhara kwa watu na mifugo hivyo kuwataka wananchi wasiwe na wasiwasi pale wanapoona wataalamu wa afya wakiweka viuadudu hivyo kwenye madimbwi na mabwawa. 

“Ushiriki wa jamii ni nguzo muhimu katika kutokomeza malaria.Ili kufanikisha zoezi la upuliziaji wa viuadudu ni lazima jamii ishirikishwe ili kuepuka mitazamo hasi kuhusu zoezi hili. Shirikisheni Viongozi wa serikali za mitaa,vijiji na kata,viongozi wa mila na dini na vikundi vya ngoma vinavyokubalika ili kutokomeza malaria”,alisema Kahundi. 

Kahundi alisema Maambukizi ya ugonjwa wa malaria katika Mkoa wa Shinyanga ni asilimia 6.1 na kitaifa ni asilimia 7.3 huku halmashauri ya wilaya ya Ushetu ikiongoza kwa kiwango cha asilimia 11.1% katika mkoa wa Shinyanga. 

“Hali ya kiwango cha maambukizi ya malaria katika mkoa katika halmashauri ya Ushetu ni 11.1%, Shinyanga 6.9%,Msalala 6.2%,Kahama Mji 3.7%, Manispaa ya Shinyanga 3.1% na Kishapu 2.9%”,alisema Kahundi. 

“Ugonjwa wa Malaria umekuwa ni ugonjwa uliozoeleka, wananchi wamesahau kwamba ugonjwa wa malaria unaua sana kwa muda mfupi mara tu usipopata matibabu kwa haraka, Malaria hupunguza nguvu kazi, kupoteza rasilimali, mahudhurio hafifu mashuleni, kupoteza maisha kwa wajawazito na kuharibika kwa mimba au kujifungua kabla ya wakati”,alieleza Kahundi. 

Alisema mkoa wa Shinyanga unaendelea kupambana na ugonjwa wa malaria kwa njia mbalimbali ikwemo kuharibu mazalio ya mbu, kutumia vyanadarua vyenye viuatilifu kuwapa elimu wananchi elimu kuhusu malaria. 

Akitoa taarifa ya hali ya Malaria katika mkoa wa Shinyanga, Mratibu wa Malaria Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Daniel Mzee alisema lengo la zoezi la Upuliziaji wa Viua Dudu ‘Larviciding’ katika mazalia ya mbu ni kutekeleza agizo lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu moja ya mikakati ya kupambana na ugonjwa wa malaria nchini ili kutekeleza kauli mbiu ya ‘Ziro Malaria inaanza na mimi’ 

Dkt. Mzee alisema jumla ya wahudumu wa afya 35 kutoka kata zote za halmashauri ya Ushetu wamepatiwa mafunzo ya namna ya kupulizia viua dudu kwa ufadhili wa asasi ya T- MARC Tanzania wanaotekeleza mradi wa 'Badilisha Tabia Tokomeza Malaria' kwa ajili ya kuhamasisha jamii kupambana na ugonjwa wa malaria katika halmashauri za wilaya za Ushetu, Msalala na Kishapu. 

Alieleza kuwa maambukizi ya malaria yanatokana na wananchi wengi kutotumia vyandarua vyenye viuatilifu,elimu duni kuhusu malaria,usafi wa mazingira na imani potofu juu ya matumizi ya vyandarua. 

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Rashid Mfaume aliwakumbusha wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kutenga fedha za kutosha katika mipango ya halmashauri za kununulia dawa za viua dudu ili zoezi la kupulizia viua dudu liwe endelevu katika halmashauri zote za mkoa wa Shinyanga. 

Naye Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC Tanzania, Hamid Al- Alawy aliiomba serikali kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii waliopatiwa mafunzo na T -MARC Tanzania ili hata watakapomaliza kutekeleza mradi wao wa 'Badilisha Tabia Tokomeza Malaria' kazi ya kupambana na malaria iwe endelevu. 

“Wahudumu hawa wa afya tumewapa ujuzi na utaalamu wa kutosha.T MARC inaahidi kutoa dawa na vifaa vya kuanzia katika zoezi la upuliziaji viua dudu katika halmashauri ya Ushetu”,alisema Alawy. 

Mmoja wa watoa huduma za afya waliopata mafunzo hayo, Shema Lupiga alisema mafunzo hayo yalifanyika kwa nadharia na vitendo kuanzia Desemba 18 hadi Desemba 21,2019 kuhusu namna ya kuendesha zoezi Upuliziaji wa Viua Dudu katika mazalia ya mbu. 

Aliyataja baadhi ya maeneo ya mazalia ya mbu ‘viluilui vya mbu’ kuwa ni mashamba ya mpunga,mabwawa,mashimo ya choo,makopo na madimbwi. 
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Mohammed Kahundi (mwenye suti nyeusi) akizindua zoezi la Upuliziaji wa Viua Dudu ‘Larviciding’ katika mazalia ya mbu mkoa wa Shinyanga kwa kupulizia dawa ya viua dudu katika bwawa la Shunu lililopo katika Halmashauri ya wilaya ya Kahama Mji leo Jumamosi Desemba 21,2019.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Mohammed Kahundi (mwenye suti nyeusi) akiendesha zoezi la Upuliziaji wa Viua Dudu ‘Larviciding’ katika bwawa la Shunu lililopo katika Halmashauri ya wilaya ya Kahama Mji.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Mohammed Kahundi (katikati) akichota maji katika bwawa la Shunu lililopo katika Halmashauri ya wilaya ya Kahama Mji ili kuangalia aina na idadi ya viluilui vilivyopo kwenye bwawa la maji.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Mohammed Kahundi na wadau mbalimbali wa afya wakiwa katika bwawa la Shunu wakati wa kuzindua zoezi la Upuliziaji wa Viua Dudu ‘Larviciding’ katika mazalia ya mbu mkoa wa Shinyanga.
Awali Afisa Afya halmashauri ya Ushetu Genoveva Gabriel akitoa ufafanuzi namna ya kuendesha zoezi la Upuliziaji wa Viua Dudu ‘Larviciding’ katika mazalia ya mbu. 
Mhudumu wa afya ngazi ya jamii kutoka kata ya Ulewe,Brown Christian akiendelea na zoezi la Upuliziaji wa Viua Dudu ‘Larviciding’ katika bwawa la Shunu. 
Kulia ni Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC, Hamid Al- Alawy akimweleza jambo Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Mohammed Kahundi wakati wa uzinduzi wa zoezi la Upuliziaji wa Viua Dudu ‘Larviciding’ katika mazalia ya mbu mkoa wa Shinyanga kwa kupulizia dawa ya viua dudu katika bwawa la Shunu lililopo katika Halmashauri ya wilaya ya Kahama Mji.Wa kwanza kushoto ni Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Rashid Mfaume.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Mohammed Kahundi akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la Upuliziaji wa Viua Dudu ‘Larviciding’ katika mazalia ya mbu mkoa wa Shinyanga.
Awali Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Mohammed Kahundi akizungumza na watoa huduma za afya ngazi ya jamii na wadau wa afya katika Ukumbi wa Kahama Super Logde Mjini Kahama. Kahundi alisisitiza elimu kuhusu udhibiti wa ugonjwa wa malaria iendelee kutolewa kwa njia mbalimbali zikiwemo wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii, Vituo vya afya, katika kaya na kwa njia ya vyombo vya habari. 
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Mohammed Kahundi akielezea mikakati inayotumika mkoani Shinyanga kutokomeza malaria kuwa ni Upuliziaji wa Viua Dudu katika mazalia ya mbu,upatikanaji wa vyandarua kwa wajawazito na watoto wanaopata chanjo ya surua / rubella, upatikanaji wa dawa ya SP kwa wajawazito kliniki, vyandarua shuleni, upimaji wa vimelea vya malaria kwa wanaohisi kuwa na homa kwa kutumnia mRDT`s na upatikanaji wa dawa mseto ya malaria.
Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC, Hamid Al- Alawy akielezea namna wanavyoshirikiana na serikali ya mkoa wa Shinyanga katika kupambana na malaria.
Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC Tanzania, Hamid Al- Alawy alisema asasi yake itatoa dawa na vifaa kusaidia kufanikisha zoezi la upuliziaji wa viua dudu katika mazalia ya mbu kwenye halmashauri ya Ushetu.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Rashid Mfaume akiipongeza na kuishukuru asasi ya T MARC Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya malaria na kuwaomba kutekeleza mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria katika halmashauri ya Shinyanga ambayo inashika nafasi ya pili kwa kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria baada ya Ushetu.
Mratibu wa Malaria Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Daniel Mzee akitoa taarifa ya hali ya malaria katika mkoa wa Shinyanga. Alisema vyandarua vyenye viuatilifu vinapatikana katika vituo vyote kwa akina mama wajawazito wanaohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza na watoto wanaopata chanjo ya kwanza ya surua-rubella.
Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya,wajumbe wa timu ya usimamizi za afya mkoa na halmashauri,wadau wa maendeleo na wahudumu wa afya ngazi ya jamii wakiwa ukumbini.
Mtoa huduma za afya Shema Lupiga akielezea namna walivyonufaika na mafunzo kwa nadharia na vitendo kuhusu namna ya kuendesha zoezi Upuliziaji wa Viua Dudu katika mazalia ya mbu.
Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya,wajumbe wa timu ya usimamizi za afya mkoa na halmashauri,wadau wa maendeleo na wahudumu wa afya ngazi ya jamii wakiwa ukumbini.
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Kahama Mji,Robert Kwela akizungumza ukumbini.
Wajumbe wa timu ya usimamizi za afya mkoa na halmashauri, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na wadau mbalimbali wa afya wakiwa ukumbini.
Watoa huduma za afya waliopata mafunzo kuhusu namna ya kuendesha zoezi la Upuliziaji wa Viua Dudu katika mazalia ya mbu.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 Blog

No comments:

Powered by Blogger.