LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shinyanga wapata mradi mkubwa wa maji "kuondoa adha iliyopo"

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com 
Shirika la "Lifewater International" lenye makao yake makuu nchini Marekani limezindua mradi wa maji mkoani Shinyanga ambapo katika awamu ya kwanza utatekelezwa katika Kata tatu za Mwantini, Mwamala pamoja na Mwalukwa zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. 

Uzinduzi wa mradi huo wa maji umefanyika Oktoba 25, 2019 kwenye ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa Shinyanga ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack. 

Akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo, Mboneko amelipongeza Shirika la hilo kwa kuanzisha mradi wa maji mkoani Shinyanga ambao utaanza kutekelezwa kwenye Kata hizo ambazo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji safi na salama. 

Amesema Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli inasisitiza upatikanaji wa maji kwenye maeneo mengi ili wananchi waweze kuondokana na adha ya ukosefu wa maji safi na salama pamoja na kuugua magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji ambayo siyo salama kiafya na kubainisha mradi huo upo sehemu sahihi. 

"Tunalishukuru sana Shirika hili la Lifewater International kwa kutuletea mradi huu wa maji mkoani Shinyanga na kuanza kutekelezwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambapo tunaomba mradi huu pia ufike na kwenye maeneo mengine ambayo yana shida ya maji safi na salama ikiwemo Wilaya ya Kishapu" amesema Mboneko. 

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Lifewater International Tanzania, Devocatus Kamara amesema mradi huo kwa kuanza utatekelezwa kwenye Kata hizo tatu za Halmshauri ya Wilaya ya Shinyanga ambazo ni Mwantini, Mwamala na Mwalukwa na baada ya hapo utapanuka kwenye maeneo yote ya Mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine ambayo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi, salama na usafi wa mazingira.

Amesema mradi huo utadumu kwa muda wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 na utagharimu zaidi ya bilioni nne (Tsh. 4,286,070,528) ambapo utajenga visima vipya virefu vya maji safi na salama na kuvikarabati vibovu, kujenga na kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora, kuboresha usafi wa mazingira na utahamasisha na kuhimiza ushiriki wa jamii kikamilifu ili kuhakikisha uendelevu wa mradi. 

Kwa upande wake Meneja wa Shirika Lifewater International Mkoa wa Shinyanga, Benety Malima amesema kuwa katika maeneo ambapo maji ya ziwa Victoria yamekwishafika, watafanya utaratibu wa kuendelea kuyasambaza katika maeneo yanayokusudiwa. Pia amesema maeneo ambayo yatapitiwa na mradi huo wa maji ni shule, zahanati na kwenye makazi ya watu ambapo mradi huo umelenga kufikia watu laki moja (100,000).
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Shirika la Lifewater International Tanzania, Devocatus Kamara akitoa ufafanuzi kwenye hafla hiyo. Katibu Tawala Mkoa Shinyanga, Albert Msovela akiwataka watumishi wa Serikali kutoa ushirikiano kwenye utekelezaji wa mradi huo. Wajumbe wakiwa kwenye uzinduzi huo. Katibu Tawala wa Wilaya Shinyanga, Boniphace Chambi akichangia mada kwenye kikao cha uzinduzi wa mradi huo. Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Mkoa Shinyanga, Malwa Kisibo akichangia mada kwenye uzinduzi huo. Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Wilaya Shinyanga, Emaeli Nkopi akichangia mada kwenye uzinduzi wa mradi huo. Wajumbe wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya Shinyanga, Jasinta Mboneko (katikati waliokaa) baada ya uzinduzi wa mradi huo.
Picha na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog

No comments:

Powered by Blogger.