LIVE STREAM ADS

Header Ads

SAUT: Mwalimu Nyerere hakuwa na tamaa, kujilimbikizia miradi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Cha Tanzania (SAUT) kampasi ya Mwanza kimeungana na watanzania kuadhimisha kumbukizi ya miaka 23 tangu kifo cha Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki Dunia Oktoba 14,1999.

Kongamano hilo lilifanyika Oktoba 14,2022 katika ukumbi wa Chuo cha SAUT Mwanza likiwajumuisha viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, wazee maarufu, machifu, walimu na wanafunzi.

Akizungumza wakati wa kufungua kongamano hilo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Cha SAUT Taaluma, Prof. Hosea Rwegoshora alisema ni kuenzi na kutafakari falsafa na mitizamo ya Mwalimu Nyerere ili kuibua mijadala mbalimbali itakayosaidia kurithisha historia kwa vizazi vinavyoendelea kukua ili kufahamu masuala ya utawala na uongozi.

Alisema Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa ni mtu wa kuridhika, hakuwa na tamaa ya kujilimbikizia mali/ miradi na maisha yake yalikuwa ni zawadi kwa watanzania.

Alisema misingi ya uongozi wake ilisaidia kuondoa tofauti za ukabila, dini, elimu, vipato, tamaduni na mitizamo mbalimbali na hivyo kuwaweka watanzania pamoja.

Naye Mwenyekiti wa kongamano hilo, Dkt. Jacob Mutashi ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa la EAGT Kiloleli jijini Mwanza alisema Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi ambaye hakufananishwa na mtu yoyote kutokana na uongozi wake kuwa na misingi ya kupendana, kuheshimiana na kusameheana.

"Misingi hiyo tumeendelea nayo hadi sasa na ndiyo maana Tanzania ni nchi ambayo ina amani ukilinganisha na nchi nyingine, niwaombe watanzania tuendelee kuitunza tunu ya amani tuliyopewa na Mungu" alisisitiza Dkt. Mutashi.

Kwa upande wake mwanasiasa mkongwe nchini, Stephen Wasira ambaye alikuwa mgeni wa heshima kwenye kongamano hilo alisema Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi aliyejitoa kwa ajili ya wengine, akilitumikia Taifa lake kwa upendo na uchungu mkubwa.

"Leo Tanzania tunafuraha na amani, ni kwa sababu ya Mwalimu Nyerere hivyo hatuna budi kuendelea kushirikiana, kupendana ili kudumisha mambo mazuri yote aliyoyapigania Baba wa Taifa" alisema Wasira.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Naibu Makamu Mkuu Taaluma Chuo Kikuu SAUT, Profesa Hosea Rwegoshora akizungumza kwenye kongamano hilo.
Mwenyekiti wa kongamano hilo ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa la EAGT Kiloleli jijini Mwanza, Dkt.Jacob Mutashi.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Stephen Wasira akizungumza kwenye kongamano hilo.
Washiriki wakifuatilia kongamano hilo.
Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Wanafunzi kutoka shule ya Sekondari Nganza jijini Mwanza wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na viongozi mbalimbali wakiwemo wa Chuo Kikuu SAUT.
Wanafunzi kutoka shule ya Sekondari Nganza jijini Mwanza wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na viongozi mbalimbali wakiwemo wa Chuo Kikuu SAUT.

No comments:

Powered by Blogger.