Samaki na dagaa lishe bora kwa watoto
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Dagaa waliokaangwa.
***
Na Tonny Alphonce, Mwanza
Wadau wa Uvuvi,Wamiliki wa Mitumbwi na Wavuvi kwa ujumla wameombwa kuzingatia suala la usalama wa chakula na kutenga baadhi ya mazao ya Ziwa kwaajili ya lishe ya watoto na familia nzima kwa ujumla.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wavuvi Duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 21 ya mwezi wa 11 kila mwaka,Afisa Mshauri kutoka Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO) Marry Fransis amesema pamoja na mazao hayo kuuzwa na kuwaongezea kipato wavuvi lakini ni muhimu wavuvi kutenga sehemu ya mazao hayo kama Samaki na Dagaa kwaajili ya lishe ya familia hususani kwa watoto wenye umri wa mwaka 1 hadi 8.
Marry amesema Samaki na Dagaa ni muhimu wakati wote kwa kuwa kuna virutubisho vyote muhimu ambavyo mwili wa mtoto unahitaji katika ukuaji wake na uboreshaji wa mifupa ya mtoto.
‘Ndio maana ndugu zangu Wavuvi na wachakataji wa Samaki na Dagaa tumekuwa tukiwapa elimu ya namna nzuri ya kuhifadhi Samaki na Dagaa ili chakula hiki kiwe salama kwa watumiaji wote lakini pia kuongeza thamani ya mazao hayo kutawaongezea fedha wavuvi na wachakataji’.alisema Marry
Marry pia amewataka Wavuvi wadogo wahakikishe wanazingatia suala la usalama kila wanapoingia kwenye vyombo vya uvuvi ili kujikinga na dhoruba zote zitakazo jitokeza ziwani na kusisitiza zaidi matumizi ya Maboya pamoja na Jaketi za kuzuia kuzama.
Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya lishe Herieth Kipuyo amewataka wazazi hasa wa mikoa mingine kutilia mkazo ulaji wa Samaki na Dagaa hasa kwa Watoto kwa kuwa ndani ya Samaki na Dagaaa mtoto atapata protini za kiwango cha juu.
‘Mtoto anapokula Samaki na Dagaa anaingiza protini mwilini kwa asilimia 90 ambapo mtoto akila nyama kiasi cha protini kinachoingia mwilini ni asilimia 90 kwa maana hiyo msione aibu kula Dagaaa maana wengine wanadhani Dagaa ni chakula cha masikini’. Alisema Bibi Kipuyo
Bibi Kipuyo amesema ukiachilia mbali kiwango kikubwa cha protini kinachopatikana kwenye Samaki na Dagaa lakini pia mtoto anapokula Samaki na dagaa hapati shida ya mmeng’enyo wa chakula kwa kuwa Samaki na Dagaa kwa ujumla wake wamejaa asidi muhimu za Amino ambayo ni muhimu sana pia kwa ukuaji wa ubongo na mfumo wa neva za mtoto.
Amezitaja faida nyingine za Samaki na Dagaa kwa mtoto kuwa ni virutubisho vyake hushiriki kikamilifu katika utengenezaji wa homoni na michakato ya kimetaboliki ambayo yote hayo ni sehemu ya afya ya mtoto mwenye nguvu.
Akizungumzia ulaji wa Samaki na Dagaa kwa watoto na ukuaji wa misuli ya mtoto Daktari Denis Kashaija mbobezi katika ukunga na afya ya kina mama kutoka hospitali ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure amesema uwepo wa mafuta ya Polyunsaturated ambayo ni sawa na mafuta ya OMEGA -3 na Omega -6 hutumika kutengeneza utando wa seli na husaidia kufanya upya tishu wakati zikiendelea kukua.
Dkt kashaija amesema ulaji wa Samaki na Dagaa kwa mtoto humsaidia pia kuwa na mifupa imara,meno imara pamoja na kucha nzuri kutokana na vitamini za A na B ambazo zinapatikana kwenye vyakula hivyo.
Shirika la chakula na Kilimo duniani mwaka 2020 liliibua nyaraka mpya ambayo inaonyesha umuhimu wa Samaki wadogo kama vile Dagaa katika kutokomeza njaa na kuinua kipato cha wakazi wa bara la Afrika.
Nyaraka hiyo ilionyesha kuwa Dagaa na Samaki wanaovuliwa mtoni na ziwani mara nyingi husindikwa,huuzwa na kuliwa na watu wazima na Watoto kukosa milo hiyo.
FAO wametolea mfano wa hatua ya kumpandikiza Sangara katika Ziwa Victoria ambaye licha kuchochea viwanda kwenye eneo hilo bado Dagaaa wamekuwa na nafasi kubwa zaidi katika kuinua lishe na kutoa uhakika wa chakula kwa mikoa yote ya kanda ya ziwa.
Pamoja na uwepo wa ziwa Victoria mkoa wa Mwanza bado unatatizo la udumavu miongoni mwa Watoto walio na umri wa mwaka 0 hadi miaka 08 ambapo tatizo la udumavu lipo kwa asilimia 26.2.
No comments: