LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali kuendelea kushirikiana nataasisi ya Trees for the Future

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson (katikati waliokaa mbele) akiwa na viongozi wengine, kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya kimataifa ya Trees for the Future Tanzania, Heri Rashid na kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga pamoja na wakulima waliohitimu mafunzo ya kilimo mseto yaliyotolewa na Taasisi hiyo. Katika mahafali hayo yaliyofanyika Kata ya Siuyu May 5, 2023 wahitimu hao walitunukiwa vyeti na zawadi mbalimbali. Kushoto walio simama nyuma ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Haika Masawe na Afisa Tawala wa Wilaya hiyo, Dijovison Ntangeki.


Na Dotto Mwaibale, Singida
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya kimataifa ya Trees for the Future Tanzania inayojishughulisha na kilimo mseto, kilimo endelevu kwa wakulima wenye kipato cha chini vijijini ili kutokomeza njaa, Umaskini na Ukataji wa miti, yenye makao yake makuu mkoani Singida ambayo inatekeleza mradi wa Bustani Misitu.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba katika mahafali ya wakulima 1445 waliohitimu mafunzo ya utekelezaji wa mradi wa Bustani Msitu katika Wilaya ya Ikungi.

"Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi ya Trees for future kwani imekuwa na mchango mkubwa wa kusaidia wakulima hapa mkoani kwetu hasa katika uhifadhi wa mazingira na kilimo mseto ambacho kina wasaidiawananchi kupata chakula na mbogamboga" alisema Serukamba.

Aidha, Serukamba aliwataka wananchi mkoani hapa kupanda miti katika maeneo ya kuzunguka nyumba zao na kwenye kingo za barabara na maeneo yote ya taasisi za Serikali ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za utunzaji wa mazingira na kuhifadhi vyanzo vya maji.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Heri Rashid akitoa taarifa kwa mkuu wa mkoa alisema taasisi hiyo imepanda miti ya matunda, mbao, uzio na miti ya kurutubisha udongo na kwamba ifikapo 2030 malengo yao ni kupanda miti bilioni moja.

Alisema miti hiyo ina manufaa makubwa kwa mazingira ikiwa ni pamoja na kufyonza hewa ukaa na kuzalisha hewa safi na inasaidia katika kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Rashid alisema mradi wa Bustani Msitu umekuwa chanzo cha vyakula vya aina mbalimbali vyenye lishe kwa kaya 1445 za wahitimu kupitia upandaji wa mbogamboga na miti ya matunda.

"Wakati tunaanza utekelezaji wa mradi wa Bustani Msitu wanufaika wetu walikuwa chini ya asilimia 25 tu ambao ndio walikuwa na uwezo wa kupata matunda na mbogamboga lakini hivi sasa wanufaika wapo zaidi ya asilimia 83 ambao wanapata mbogamboga na matunda ndani ya saa 48," alisema.

Alisema kupitia mradi huo ambao lengo kuu ni kuongeza uzalishaji katika shamba la mkulima, wakulima wameweza kuuza matunda yao sokoni mjini Singida kama vile pasheni na papai na hivyo kujipatia fedha ambazo zimewasaidia kuendesha maisha yao ya kila siku.

Aliongeza kuwa baada ya wakulima kuanza kunufaika na bustani zao, taasisi ya Trees for the future ilianzisha vikundi 107 vya wakulima vya huduma ndogo za fedha ambavyo vimesajili katika halmashauri za Wilaya ya Singida, Mkalama,Iramba na Ikungi.

Alisema vikundi hivyo vinawasaidia wakulima kuweka akiba na kulipa ili fedha zinazopatikana kutoka kwenye mazao ya Bustani msitu iweze kuzungushwa miongoni mwa wakulima wanufaika hali ambayo imesaidia kuinua hali zo za maisha.

Alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana kumekuwa na changamoto ya tatizo la ukame kutokana na ukanda huu kupata mvua chache, mifugo kuchungiwa kwenye mashamba ya Bustani msitu na upungufu wa fedha za kuendesha miradi.

Mnufaika wa mradi huo Juma Shabani ameishukuru taasisi hiyo kwa kumpa maendeleo katika kilimo hadi kufikia hatua ya kuingiza umeme na maji kwenye nyumba yake aliyoijenga Kata ya Mungaa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga aliiomba taasisi hiyo kuongeza miaka mingine ya kutekeleza mradi wa namna hiyo kwenye wilaya hiyo ili wananchi wengi waweze kunufaika na teknolojia hiyo ya uhifadhi wa mazingira pamoja na kilimo mseto.

Kabla ya kuanza kwa mahafali hayo RC Serukamba aliyekuwa ameongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na wataalam mbalimbali alipata fursa ya kutembea mashamba ya wanufaika wa mradi huo, Basili Mtaturu na Juma Shabani yaliyopo Kata ya Mungaa na Siuyu ambapo alijionea kazi kubwa iliyofanyika ya utunzaji wa mazingira kupitia kilimo mseto.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida,Thomas Apson (katikati) akijiandaa kukata keki maalumu iliyoandaliwa na Taasisi hiyo kwa ajili ya mahafali hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akihutubia kwenye mahafali hayo.
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Heri Rashid akimlisha keki Mkuu wa Wilaya ya Ikungi wakati wa mahafali hayo.
Mratibu wa Shirika hilo Mkoa wa Singida Ibrahim Mghama (kulia) akiongoza msafara wa mkuu wa mkoa wakati ulipotembelea shamba la mnufaika wa mradi huo, Basili Mtaturu wa Kata ya Siuyu. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Heri Rashid, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson, Mnufaikawa mradi huo, Basili Mtaturu na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Muonekano wa kebeji iliyolimwa na mnufaika wa mradi huo, Juma Shabani.
Muonekano wa mapapai katika shamba la mnufaika wa mradi huo Juma Shabani.
Afisa Uhusiano wa Taasisi hiyo Ally Juma, akizungumzia mafanikio makubwa ya mnufaika wa mradi huo, Juma Shabani.
Mnufaika wa mradi huo, Juma Shabani, akiwa shambani kwake.
Msafara wa viongozi mbalimbali ukitoka kutembelea shamba la mnufaika wa mradi huo, Juma Shabani.
Wimbo waTaifa ukiimbwa kwenye mahafali hayo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Trees for the future, Heri Rashid akitoa taarifa ya taasisi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson akizungumza kwenye mahafali hayo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga (kulia) akiwa naDiwani wa Kata ya Siuyu, Selestine Yunde katika mahafali hayo.
Burudani ya ngoma ya asili ya kabila la Wanyaturu ikitolewa.
Wafanyakazi wa taasisi hiyo wakiserebuka sanjari na wasanii wa Kata ya Siuyu wakati wa mahafali hayo.
Vyeti vikitolewa kwa wakulima wahitimu wa mafunzo ya kilimo mseto yaliyotolewa na taasisi hiyo.

No comments:

Powered by Blogger.