LIVE STREAM ADS

Header Ads

SHULE YA SEKONDARI KISHIMBA MKOANI SHINYANGA YAKABILIWA NA CHANGAMOTO MBALIMBALI.

Na:Shaban Njia
Shule ya Sekondari ya Kishimba iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Kahama Mkoani Shinyanga, inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa miundombinu ya Umeme hali inayosababisha wanafunzi wake kushindwa kujisomea vyema hususani nyakati za usiku na hivyo kuathiri ufaulu Shuleni hapo.

Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa Shule hiyo, Melkisedeck Choya wakati akisoma risala katika uzinduzi wa Maktaba ya shuleni hapo ambapo alikiri kuwa kwa kipindi ukosefu wa Umeme na Maabara katika shule hiyo umeweza kuathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wanafunzi.

Choya alisema kuwa pamoja na kuwezeshwa kuwa sekondari ya kwanza katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, kuwa na Maktaba itakayosaidia kuongeza taaluma kwa wanafunzi kwa kujisomea na kuazima vitabu vya kiada na ziada, lakini ukosefu wa miundombinu ya umeme utaendelea kuathiri ufanisi wa shule hiyo.

Alisema mbali na miundo mbinu ya Umeme, pia upungufu wa viwanja vya michezo katika shule hiyo unaathiri uibuaji wa vipaji vya vijana katika sekta hiyo ambayo katika karne hii inazalisha ajira.

Kwa upande wake Meneja wa Atlas Copco Tawi la Mwanza, Menas Ngonyani alisema kuwa ni kawaida kwa kampuni yake ambayo imekuwa ikifanya kazi katika Kanda ya ziwa tangu mwaka 2008, kurejesha pato inalozalisha kwa kusaidia huduma za jamii katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu.

Nae mzazi Asha Ally Salmu aliwasihi wanafunzi wasijinyanyapae kwa kuona wanasoma katika shule za Serikali ambazo zinadharauliwa tofauti na zile za watu binafsi (English Medium), na kuwaeleza kuwa jitihada na umakini wa kuwasikiliza vyema walimu wao ndio utakuwa dira ya mafanikio yao katika masomo na hata katika maisha yao ya baadae.

Maktaba katika shule hiyo ilijengwa na Shirika la Read International chini ya ufadhili wa Atlas Copco ambapo imegharimu kiasi cha takribani Shilingi Milioni Nane, kwa kuhusisha upakaji rangi,kutengeneza kabati za kuhifadhi vitabu,meza na viti sambamba na vitabu vya kiada na ziada kwa wanafunzi.

No comments:

Powered by Blogger.