LIVE STREAM ADS

Header Ads

DKT. CHAYA: UWEKEZAJI WA VIWANDA NI NGUZO YA AJIRA, MASOKO YA WAKULIMA NA UCHUMI WA TAIFA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Group of Companies, Mhe. Salum Khamis akieleza hatua za uzalishaji pamoja na uwekezaji uliofanyika kiwandani.
Mkurugenzi wa Kampuni ya East African Spirits (T) Limited (EASTL), Bw. Gaspar Kileo, akimuongoza Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji katika kiwanda hicho mkoani Shinyanga.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog Shinyanga

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kusisitiza uwekezaji wa viwanda wenye tija kama nguzo kuu ya kukuza uchumi wa taifa, kutengeneza ajira kwa Watanzania na kuhakikisha wakulima pamoja na wafugaji wanapata masoko ya uhakika ya mazao yao.

Dkt. Chaya ameyasema hayo leo Ijumaa Januari 9, 2026, wakati akitembelea viwanda mbalimbali vya uwekezaji mkoani Shinyanga, vikiwemo Kiwanda cha Jambo Group of Companies na Kiwanda cha Uzalishaji wa Vinywaji Vikali cha Kampuni ya East African Spirits (T) Limited (EASTL), ambapo amejionea shughuli za uzalishaji na kupongeza mchango mkubwa wa wawekezaji wazalendo katika maendeleo ya kiuchumi ya Taifa.

Akizungumza baada ya kutembelea Kiwanda cha Jambo Group, Dkt. Chaya alisema mwelekeo wa Serikali kwa sasa umejikita katika kuimarisha uwekezaji wa viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo, ili kuondoa changamoto ya masoko kwa wakulima na wafugaji na kuongeza kipato chao.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya.

“Tanzania ina wakulima na wafugaji wengi, lakini changamoto imekuwa ni masoko ya uhakika na viwanda vya kuchakata mazao. Serikali inahitaji wawekezaji kama Jambo Group wanaowekeza kwenye viwanda vinavyowagusa wananchi moja kwa moja,” amesema Dkt. Chaya.

Naibu Waziri huyo ameipongeza Jambo Group kwa mchango wake mkubwa katika utoaji wa ajira, akieleza kuwa kampuni hiyo imeajiri wafanyakazi zaidi ya 1,000 wa kudumu na takribani 10,000 wa muda, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira, hususan kwa vijana na wanawake, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Aidha, amewahimiza wawekezaji wengine wa Kitanzania kuiga mfano huo, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, kuimarisha miundombinu na kutoa ushirikiano unaohitajika ili viwanda viendelee kukua na kuongeza uzalishaji.

Akisoma taarifa ya kampuni hiyo, Mkurugenzi wa Jambo Group of Companies, Khamis Salum, amesema uwekezaji wao umejikita katika bidhaa za matumizi ya kila siku (FMCG) na umefanywa kwa kutumia mitambo ya kisasa ya viwango vya Ulaya, ili kuhakikisha uzalishaji wenye ubora, ufanisi na usalama wa bidhaa.

Ameeleza kuwa Jambo Group of Companies ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa nchini na imeendelea kutoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya watu 1,000 pamoja na ajira zisizo za moja kwa moja kwa zaidi ya 10,000 kupitia mnyororo wa thamani. 
Mkurugenzi wa Jambo Group of Companies, Khamis Salum

Aidha, miradi yao ya maziwa yenye uwezo wa kuchakata hadi lita 100,000 kwa siku imekuwa soko la uhakika kwa wafugaji, ikitoa bei za ushindani, malipo kwa wakati na mafunzo ya ufugaji wa kisasa.

Kupitia vituo vya kukusanyia maziwa vilivyosambaa vijijini na katika miji midogo, kampuni hiyo imepunguza upotevu wa mazao, kuondoa hofu ya kukosa wanunuzi na kuongeza kipato cha kaya za wafugaji, huku ikiendelea kutoa mafunzo ya lishe bora ya mifugo, usimamizi wa malisho, pamoja na kinga na tiba ya magonjwa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Chaya ametembelea Kiwanda cha East African Spirits (T) Limited (EASTL)  LTD na kupongeza uwekezaji mkubwa wa mwekezaji mzawa, Bw. Gaspar Kileo, akisema ni mfano halisi wa uzalendo wa kiuchumi unaotekeleza kwa vitendo sera ya Serikali ya kukuza uchumi wa viwanda.
“Nichukue fursa hii kumpongeza mwekezaji mzawa Gaspar Kileo kwa kuamua kuwekeza hapa nyumbani badala ya kupeleka mtaji nje ya nchi. Amewekeza zaidi ya shilingi bilioni 30, ameweka mitambo ya kisasa na maabara ya viwango vya juu,” amesema Dkt. Chaya.

Kwa mujibu wa taarifa alizopewa, kiwanda cha EASTL kinachangia zaidi ya Shilingi Bilioni 20 kwa mwaka kama kodi kwa Serikali na kimezalisha ajira zaidi ya 200 za moja kwa moja, sambamba na ajira zisizo za moja kwa moja kupitia mnyororo wa thamani.

Naibu Waziri ameeleza kuwa uzalishaji wa bia, wine na spirit unategemea malighafi kama shayiri (barley), inayolimwa na wakulima kutoka maeneo mbalimbali hususan Kanda ya Kaskazini, jambo linalochochea sekta ya kilimo na kuongeza kipato cha wakulima.

“Huu ni uwekezaji unaogusa maisha ya wananchi wengi. Unakuza kilimo, unazalisha ajira kwa waliosoma na wasiosoma, na unaongeza mapato ya taifa. Hii ndiyo adhima ya Serikali ya Awamu ya Sita,” ameongeza.

Katika maelezo yake, Dkt. Chaya amebainisha pia changamoto ya upungufu wa chupa za kufungashia vinywaji, akisema ni fursa kubwa ya uwekezaji kwa Watanzania. 

Ameeleza kuwa kwa sasa mwekezaji wa chupa nchini yupo Dar es Salaam pekee, hali inayotoa mwanya mkubwa kwa wawekezaji wengine kuwekeza katika sekta hiyo, hususan kupitia mpango wa Serikali wa kuanzisha Kongani za Viwanda katika kila wilaya.

“Tunapofuatilia uwekezaji, tunaangalia mambo matatu: je uwekezaji una tija, je unazalisha ajira, na je unahusisha mnyororo wa thamani na kukuza pato la taifa. Uwekezaji wa Jambo Group na EASTL unakidhi vigezo vyote hivyo,” amesisitiza.
Awali, akisoma risala ya uongozi wa East African Spirits (T) Ltd kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi Msaidizi wa Masoko na Uongozi wa kampuni hiyo, Godbless Gaspar Kileo, amesema kuwa ujio wa Naibu Waziri unaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwawezesha na kuwaunga mkono wawekezaji wazalendo.

Amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ulianza Oktoba 2019 kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao ya kilimo mkoani Shinyanga, na kwamba baada ya kukamilika kwa ujenzi na usimikaji wa mitambo, kiwanda kilizinduliwa rasmi Machi 2023 na kuanza uzalishaji kwa kuzingatia viwango vya ubora na ushindani wa soko.

Kileo amesema kuwa hadi sasa uwekezaji katika mradi huo umefikia Shilingi bilioni 34, kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo Benki ya CRDB, na kwamba manufaa yake yamejidhihirisha kupitia ajira zaidi ya 200 za moja kwa moja, ongezeko la mapato ya Serikali na kukuza kipato cha wakulima wa shayiri kutoka Hanang, West Kilimanjaro na Siha.

Ameongeza kuwa kiwanda hicho pia kimekuwa kikichochea uchumi wa ndani kwa kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi wanaokizunguka, wakiwemo Mama Lishe, wabeba mizigo na watoa huduma wadogo wadogo katika Manispaa ya Shinyanga.

Amesema uongozi wa East African Spirits (T) Ltd unaomba Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wazalendo ili kuongeza uzalishaji, kupanua masoko ya ndani na nje ya nchi, na kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa.

Katika ziara hiyo, Dkt. Chaya pia ametembelea Kiwanda cha Nyama kilichopo Old Shinyanga, ambapo amesema eneo hilo lipo wazi kwa uwekezaji na kuwataka wawekezaji kujitokeza kuwekeza.

Mkurugenzi wa Kampuni ya East African Spirits (T) Limited (EASTL), Bw. Gaspar Kileo, akimkaribisha Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, kabla ya kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji katika kiwanda hicho mkoani Shinyanga.
Mkurugenzi Msaidizi wa Masoko na Uongozi wa Kampuni ya East African Spirits (T) Limited (EASTL), Bw. Godbless Gaspar Kileo, akisoma risala ya uongozi wa kampuni hiyo kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, wakati wa ziara katika kiwanda hicho mkoani Shinyanga.
Mkurugenzi wa Kampuni ya East African Spirits (T) Limited (EASTL), Bw. Gaspar Kileo, akimueleza Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya (kulia), kuhusu mchakato wa uzalishaji wa vinywaji katika kiwanda hicho.
Mkurugenzi wa Kampuni ya East African Spirits (T) Limited (EASTL), Bw. Gaspar Kileo, akimuongoza Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji katika kiwanda hicho mkoani Shinyanga.
Mkurugenzi wa Kampuni ya East African Spirits (T) Limited (EASTL), Bw. Gaspar Kileo, akimuongoza Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji katika kiwanda hicho mkoani Shinyanga.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, alipotembelea kiwanda cha Kampuni ya East African Spirits (T) Limited (EASTL) mkoani Shinyanga.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, pamoja na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, wakionesha bidhaa za maziwa zinazozalishwa na Kiwanda cha Jambo wakati wa ziara yao ya kikazi.
Mkurugenzi wa Jambo Group, Khamis Salum, akisoma taarifa fupi ya kampuni hiyo leo Ijumaa, Januari 9, 2026, wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, katika kiwanda hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Group, Mhe. Salum Khamis Mbuzi, akieleza mchango wa kiwanda hicho katika uundaji wa ajira, ulipaji wa kodi na kukuza maendeleo ya sekta ya maziwa, wakati wa ziara ya viongozi wa Serikali mkoani Shinyanga
Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Group, Mhe. Salum Khamis, akiwaongoza viongozi wa Serikali na Mkoa wa Shinyanga kutembelea maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho, akieleza hatua za uzalishaji pamoja na uwekezaji uliofanyika.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya akizungumza alipotembelea Kiwanda cha Nyama kilichopo Old Shinyanga, ambapo amesema eneo hilo lipo wazi kwa uwekezaji na kuwataka wawekezaji kujitokeza kuwekeza.




No comments:

Powered by Blogger.