LIVE STREAM ADS

Header Ads

TCCIA YAWAOMBA WAFANYABIASHARA KUSHIRIKI MAONYESHO YA BIASHARA YA AFRIKA MASHARIKI.

Judith Ferdinand na Getruda Ntakije
Wafanyabiashara nchini wameombwa kushiriki katika maonyesho ya biashara ya kimataifa ya Afrika Mashariki, ili kukuza ushirikiano, kujifunza na kupanua wigo kibiashara kutoka nchi jirani.

Maonyesho hayo yanatoa fursa kwa wafanyabiashara nchini, kuonyesha bidhaa zao na huduma wanazotoa kwa umma, ili waweze kukuza biashara na kupata mawakala nchi nzima na jirani ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Wito huo ulitolewa juzi na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda  na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Mwanza, Elibariki Mmari kwenye uzinduzi wa maonyesho ya 10 ya  biashara ya Afrika Mashariki yanayofanyika katika uwanja wa chuo cha Dar es Salaam Institute of Technology (D.I.T) tawi la Mwanza.

Mmari aliwataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa zilizopo kwa kujitangaza kupitia maonyesho mbalimbali, ili kuweza kukuza uchumi na kuleta ushindani katika soko la Afrika Mashariki na dunia.

“ Kujitangaza ndio njia pekee ya kuonyesha fursa za kiuchumi tulizonazo na kukuza biashara zetu, hii ni kutokana na uchumi wa nchi za Afrika Mashariki kukua kwa  kasi huku shughuli za kibiashara zikiendelea". Alisema Mmari na kuongeza;

“Sisi TCCIA tunapenda kuwahimiza wafanyabiashara wetu kujenga tabia ya kushiriki kwenye maonyesho ya biashara, kwa kuwa ni sehemu ambayo anapata fursa ya kutangaza bidhaa zake, kupanua wigo wa wateja pamoja na kupata masoko mapya".

Hata hivyo aliiomba serikali kufadhili maonyesho hayo, ili wajasiriamali waweze kushiriki  na kunufaika na soko la Afrika Mashariki kutokana na gharama za mabanda kupanda kila mwaka.
Bonyeza HAPA Kuona Picha

No comments:

Powered by Blogger.