LIVE STREAM ADS

Header Ads

MIAKA MINANE TANGU UTANGULIE MBELE ZA HAKI MZEE WETU MARWA BINAGI, BADO TUNAKUKUMBUKA.

"Yapo mengi ya kusema ila kwa leo nasema, pengo uliloliacha Mzee wetu Daniel Marwa Binagi tangu tarehe 06.02.2008 bado linaonekana na halitasahaulika kamwe. Mwenyezi Mungu Ailaze Roho yako Pahala Pema Peponi, Amina! Ni mimi mwanao Mpendwa
George Marwa Binagi (Pichani)".
Mwaka jana liniandika, Ilikuwa ni Sekunde, Dakika, Masaa, Siku, Wiki, Mwaka hatimae hivi sasa ni miaka (miaka Minane mwaka hu) imepita tangu ututoke duniani Baba yetu Mpendwa, huku ukiacha kilio na majonzi kwa wanao tuliokuwa bado wachanga ambao hakika ulituacha ilihali tukihitaji malezi yako.

Ukiwa na Miaka 83 mwaka 2008, Mzee wetu Mzee Daniel Marwa Binagi Mzaliwa na Mkazi wa Kitongoji cha Chira Kata ya Turwa (Zamani), hivi sasa Kata ya Kenyamanyori Wilaya ya Tarime Mkoani Mara Mwenyezi Mungu alikupenda zaidi na kukuchukua ili ukapumzike baada ya kuteseka kwa maradhi katika kipindi cha muda mrefu.

Hakika uliipenda na kuiongoza Familia yako bila ubaguzi wa aina yoyote. Ulionyesha Mapenzi tele si tu kwa Wanao, Wajukuu zako, Wake zako bali kwa kila mmoja aliekuzunguka ambapo uliweza kuonyesha mapenzi tele kwake huku tabia yako ya kuchukia upuuzi na kuukumbatia ukweli ukikuongezea sifa rukuki kwa waliokufahamu.

Ukiwa na Elimu ya darasa la nne ambayo uliipata enzi za Mkoloni, uliweza kuleta mapinduzi ya ajabu katika Kijiji chako na hata Wilaya ya Tarime na kuwa mmoja wa Watu wenye Mafanikio makubwa Wilayani Tarime si tu kwa Kuwekeza katika Ujenzi wa nyumba na Biashara katika mji wa Tarime bali hata katika Uungwana wako.

Ulijizolea sifa ya kuhakikisha kila mtoto anapata elimu kadri apendavyo na hivyo ndivyo ilivyokuwa na ndiyo maana wakapatikana vijana mbalimbali kutoka katika uzao wako wakiwa nafasi mbalimbali za utumishi ikiwa ni pamoja na wale walioingia katika Sekta ya Elimu, Afya, Habari, Biashara, Urubani ikiwa ni miongoni mwa taaluma mbalimbimbali huku wewe mwenyewe ukiamini katika mfumo wa Biashara, Kilimo na Ufugaji.

Hakika wote waliopata malezi yako wanajivunia mpaka leo kuwa na Mzazi kama wewe Mzee wetu Daniel Marwa Binagi. Nakumbuka mambo mengi sana kutoka kwako ambayo ulikuwa ukiwatendea wakati huo mimi nikiwa mdogo. 

Nilitamani sana kupata malezi yako lakini Mwenyezi Mungu alikupenda zaidi. Nakumbuka namna ndugu zangu walivyosoma katika Shule na Vyuo vizuri tena kwa gharama kubwa. Naogopa kusema sana ili nisije nikakufuru ila nina kila sababu ya kusema kwamba pengine nami ningekuwa mmoja wa wanao ambao wangesoma katika shule na vyuo vizuri kama ulivyokuwa ukiniahidi wakati ukiwa kitandani unauguza maradhi yaliyokuwa yakikusibu.

Hakika Mzee wetu wetu Daniel Marwa Binagi tututaendelea kukukumbuka kwa kuyaendeleza yale yote mazuri uliyotuachia licha ya changamoto nyingi zinazojitokeza kutokana na pengo lako. Yapo mengi ya kusema ila kwa leo nasema kwamba pengo uliloliacha tangu tarehe 06.02.2008 bado linaonekana na halitasahaulika kamwe. Hakika safari uliyoianza hapa duniani tangu tarehe 25.02.1925 ilifikia tamati mwaka huo wa 2008. Mwenyezi Mungu Ailaze Roho yako Pahala Pema Peponi, Amina! 
Ni mimi mwanao Mpendwa 
George Marwa Binagi.

No comments:

Powered by Blogger.