LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAZIRI NAPE ATAJA WALIOIREJESHA CCM MADARAKANI 2015.

Na Daniel Mbega
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, amekiri kwamba, mitandao ya kijamii hususan blogu, ndiyo imekirudisha madarakani Chama cha Mapinduzi – CCM.

Akizungumza jana jijini dar es salaam wakati wa ufungaji wa semina na mkutano mkuu wa Chama cha Mabloggers Tanzania – yaani Tanzania Bloggers Network – TBN , Nape alisema kwamba, katika kipindi ambacho CCM ilikuwa inaonekana kuchukiwa na baadhi ya wananchi na kutishiwa uwezekano wa kurudi madarakani, ni bloggers ndio walikuwa muhimili mkubwa wa kurejesha imani kwa wananchi hata wakaichagua tena.

‘Wakati nikiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, na wakati ambao ulikuwa mgumu zaidi kwa serikali ya CCM, ambapo ilikuwa ikishambuliwa na upinzani, ni bloggers ambao walisimama imara na kuandika ukweli kuhusu serikali ya CCM kiasi cha kurudisha imani ya wananchi na hatimaye tukampata Rais john Magufuli,’ alisema Nape.

Waziri Nape alibainisha kwamba, mitandao ya kijamii ni zaidi ya vyombo vya habari vingine kwa kuwa ndiyo inayoanza kuchapisha taarifa kabla hata ya vyombo vingine vya kawaida kuziripoti, hivyo akasema serikali inaitambua na kuiunga mkono.

Aidha, alisema kwamba, kwa kuwa hivi sasa Watanzania takriban milioni 21 wanatumia mtandao wa internet, ni muhimu kutambua na kuipa kipaumbele mitandao mitandao ya kijamii kama blogu, ambayo kwa kiasi kikubwa imeunganishwa na mitandao mingine kama facebook na twitter.

‘Facebook ina watumiaji karibu milioni tatu, twitter ina watumiaji zaidi ya milioni moja na nusu pamoja na mitandao mingine, lakini hii yote imeunganishwa kwenye blogu, hivyo kuna kila sababu ya kuthamini mchango wa mitandao ya kijamii na endapo itatumiwa vyema, inaweza kuleta manufaa kwa umma kwa kusukuma mbele gurudumu la maendeleo,’ alisema.

Aliwahakikishia bloggers kwamba, serikali inawatambua, inawathamani na inaunga mkono juhudi zao katika upashanaji habari na kwamba serikali iko tayari kuwasaidia kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa uhuru na kwa weledi.

Aliongeza kusema kwamba, wanamitandao hao wako huru kuikosoa serikali katika kujenga na kwamba taarifa nyingi wanazoziandika zinafanyiwa kazi na serikali japokuwa siyo rahisi kuona moja kwa moja.

Katika kuthibitisha kuwaunga kwake mkono, Waziri Nape ameuagiza uongozi wa TBN kuanzisha Tuzo za Blog Bora kuanzia mwakani na kwamba zinaweza kuwekwa katika makundi mbalimbali, hatua ambayo siyo tu itawahamasisha wanamitandao wenyewe, bali pia itawafanya wajikite katika maeneo mbalimbali na kufanya kazi kwa makini zaidi badala ya sasa ambapo walio wengi hawajajipambanua kwamba wako upande gani.

‘Ninawaagiza muanzishe mara moja tuzo hizi kama wenzetu Wakenya, mkijipambanua maeneo yenu mtafanya kazi kwa ufanisi na itasaidia kuleta maendeleo ya taifa,’ alisema na kuongeza kwamba, wizara yake itasaidia kwa namna moja ama nyingine kuhimiza hata baadhi ya taasisi za serikali ziweze kudhamini tuzo hizo.

Wanachama wa TBN walikuwa katika semina na mkutano wao maalum wa mwaka ambao ulifanyika jijini Dar es Salaam tangu Jumatatu Desemba 5 hadi Jumanne Desemba 6, 2016.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makonda, amesema anautambua mchango mkubwa wa bloggers wa Tanzania na kwamba wanamsaidia katika kutekeleza majukumu yake ya serikali.

‘Bloggers wanajitahidi kuripoti habari nyingi na kwa wakati, zipo habari ambazo katika vyombo vingine vya habari zinaweza zisiripotiwe, lakini bloggers wanaziandika kwa mapana na kwa wakati, hivyo kwangu mimi vyombo hivi vya mitandao ni muhimu na niko tayari kusaidia wakati wowote mtakaponihitaji,' Makonda alimweleza Mwenyekiti wa TBN, Joachim Mushi, kwa njia ya simu wakati mkutano huo ukiendelea.

No comments:

Powered by Blogger.