DKT.ANGELINA MABULA AAHIDI WATAALAMU WA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI SINGIDA.
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.
Naibu
Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akizungumza na
wataalamu wa ardhi, viongozi na watendaji wa halmashauri ya Wilaya na Manispaa
ya Singida (hawapo pichani), Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi.
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi imeahidi kutoa timu ya wataalamu watakao suluhisha mgogoro wa mpaka kati
ya Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida na Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara.
Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angelina Mabula ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara yake Mkoani Singida katika
kijiji cha Singa tarafa ya Kinampundu Wilayani Mkalama ambapo amesema Wizara
yake itatoa wataalamu watakaoweza kutatua mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya
miaka 30.
“Kwakuwa pande zote mbili za Mkalama na Hanang’ zimekutana
mara kadhaa bila mafanikio, nitaleta wataalamu wafike eneo la mpaka ili
wataalam hao wawasomee alama moja baada ya nyingine, kila mmoja wenu afahamu
eneo lake mwisho ni wapi, nadhani hapo tutakuwa tumewasaidia wananchi wetu”,
amesema Dkt Mabula.
Amesema wananchi wa Kijiji hicho cha Singa wasiwe na
wasiwasi endapo baada ya kuonyesha mpaka wao mashamba yao yakionekana yapo
wilaya ya Hanang’ wataruhusiwa kuendelea kuyamiliki ila watatakiwa kwenda
kujitambulisha katika Uongozi wa Wilaya hiyo.
Aidha Dkt Mabula amesema timu hiyo ya wataalamu itahakikisha
inasuluhisha migogoro yote ya mipaka ya wilaya hiyo ambayo ngazi ya wilaya
imeshindikana kutatuliwa.
Amewashauri wananchi hao kutouza au kugawa ardhi yao ovyo
ovyo kwakuwa ardhi ni mali na mtaji popote pale hata kama ni vijijini hivyo
watunze ardhi yao na kuiongezea thamani kwa kuipima na kuwa na hati ya umiliki.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walitoa malalamiko kwa
Naibu Waziri huyo huku wakimueleza kuwa mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu
umesababisha baadhi yao kupelekwa mahakamani kwa madai ya kuvamia mashamba.
Mzee Anaftali Amosi Majii amemueleza Naibu waziri kuwa
taarifa za mgogoro huo zilitolewa muda mrefu na kuongeza kuwa wananchi
wamechoka kushitakiwa kwa makosa ya uvamizi wa mashamba wakati wao wanaamini
wanayamiliki kwa uhalali jambo ambalo linawachelewesha kimaendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama
Mhandisi Geofrey Sanga amesema Wilaya ya Mkalama ina migogoro ya mipaka kwa
wilaya tano zinazowazunguka.
Mhandisi Sanga ameeleza kuwa Mkalama ina migogoro ya mipaka
kati yake na Wilaya za Mbulu, Iramba, Hanang’ na Wilaya ya Singida jambo ambalo
linawafanya baadhi ya wananchi kukwepa kuchangia shughuli za maendeleo wakidai
wao sio wa Wilaya hiyo.
Wakati huo huo Naibu Waziri Dkt Angelina Mabula amefanya
ziara Wilaya ya Iramba na kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika masijala ya
Ardhi ya Wilaya hiyo ambapo hakuridhishwa na utunzaji wa nyaraka pamoja na
utendaji usioridhisha unaosababisha wananchi kuchelewa kupata hati za viwanja.
Dkt Mabula pia hakuridhishwa na kasi ndogo ya upimaji
viwanja na utoaji wa hati wilayani humo huku akiwataka kuacha kukusanya kodi
mbalimbali za ardhi kwa utendaji wa kimazoea bali wafanye kazi bidii.
Naibu
Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akizungumza na
wananchi wa kijiji cha Singa tarafa ya Kinampundu Wilayani Mkalama, Kulia kwake
ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jaksoni Massaka.
Naibu
Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akisikiliza
maelezo kutoka kwa Afisa Ardhi wa Wilaya ya Iramba Lugano Sanga kuhusu utuzanji
wa nyaraka za idara hiyo.
Naibu
Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akimkabidhi
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi hati ya kumiliki kiwanja chake
kilichopo Mjini Dodoma.
Na RAS Singida
No comments: