LIVE STREAM ADS

Header Ads

TRA Mkoa Mwanza yaongeza kasi ukusanyaji mapato

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com 
Judith Ferdinand, BMG
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa Mwanza imeongeza kasi ya ukusanyaji mapato ambapo katika kipindi cha mwezi Julai na Agosti mwaka wa fedha 2019/20, imekusanya shilingi bilioni 10.8 ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2017/18 ambapo ilikusanya shilingi bilioni 8.3.

Meneja wa mamlaka hiyo, Joseph Mtandika ameyasema hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara wanaotumia bandari za Mwanza pamoja na uwanja wa ndege wa Mwanza kusafirisha bidhaa zao.

"Ongezeko hilo limekuja baada ya kuanza kutumia usafiri wa majini kusafirisha bidhaa mbalimbali kupitia bandari za Mwanza" amebainisha Mtandika.

Akizungumza na wafanyabiashara wanaotumia bandari na uwanja wa ndege kusafirisha bidhaa zao Meneja TRA Mkoa wa Mwanza,Joseph Mtandika alisema baada ya kuanza kutumika kwa bandari hiyo kusafirisha bidhaa pato limeongezeka.

Naye mmoja wa wafanyabiashara mkoani Mwanza, Brown Mushi ametoa rai kwa wafanyakazi wa forodha pamoja na jeshi la polisi kushirikiana ili kuondoa usumbufu wanaopitia wakati wa usafirishaji wa bidhaa zao.

"Wafanyabiashara tunashindwa kuaminika na baadhi ya mamlaka katika mazingira tunayofanyiwa ukaguzi hivyo inatusababishia kucheleweshwa njiani kwa kukamatwa na askari wa usalama barabarani wakidai baadhi ya nyaraka na hata tukiwapa hawana ujuzi wa kuzielewa na hivyo kutusababishia usumbufu" ameeleza Mushi

Naye Meneja Msaidizi wa Forodha Mkoa wa Mwanza, Christopher Sojo amesema soko la Afrika Mashariki lina unafuu wa kodi kwa bidhaa ambazo zimetengenezwa ndani ya nchi za ukanda huo hivyo ni fursa kwa wafanyabiashara kutumia bandari ya Mwanza Kusini ili kupunguza gharama za biashara.

"Tungependa kuwa na wafanyabiashara ambao hawajihusishi na magendo wala biashara haramu na ikitokea hivyo wafanyabiashara wengine watoe taarifa katika mamlaka husika ili hatua za kisheria zichukuliwe ili kuhakikisha mapato ya nchi hayapotei" amesisitiza Sojo.

No comments:

Powered by Blogger.