LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Biteko aitaka kampuni ya Mantra Tanzania kuwa na subira

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Waziri wa Madini, Doto Biteko akiwakaribisha wajumbe kutoka kampuni ya Mantra Tanzania pamoja na wataalamu wa Wizara hiyo katika kikao kilichoketi Oktoba 01, 2019 jijini Dodoma kikilenga kujadili uchimbaji wa madini ya Uranium hapa nchini.
#BMGHabari
Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Augustine Ollal akihoji jambo wakati wa kikao baina ya Wizara ya Madini pamoja na kampuni ya Mantra Tanzania kilichofanyika katika Ofisi ya Waziri wa Madini, Doto Biteko.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mantra nchini, Frederick Kibodya akizungumza jambo wakati wa kikao baina ya kampuni hiyo na Wizara ya Madini kilichoongozwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Uranium One, Alexander Ryabchenko wakati akizungumza jambo kwenye kikao hicho. 
Waziri wa Madini, Doto Biteko pamoja na wajumbe walioshiriki kikao baina ya Wizara ya Madini pamoja na kampuni ya Mantra Tanzania wakifurahia jambo wakati kikao hicho kikiendelea.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mantra Tanzania, Alexander Ryabchenko akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza jambo na Rais wa kampuni ya Uranium One, Vasiliy Konstantinov.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Uranium One, Alexander Ryabchenko baada ya kumaliza kikao baina ya Wizara ya Madini pamoja na kampuni hiyo. Katikati ni Rais wa kampuni hiyo, Vasiliy Konstantinov.


Na Nuru Mwasampeta, Wizara ya Madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko, ameitaka kampuni ya Mantra Tanzania kuipa nafasi ofisi yake ili kujiridhisha endapo maombi ya kusitisha kuanza kwa shughuli za uchimbaji wa madini ya uranium una tija kwa kampuni na Taifa.

Waziri Biteko alitoa kauli hiyo Oktoba 01, 2019 wakati wa kikao baina ya Wizara ya Madini na uongozi wa kampuni hiyo ulioitaka Wizara kuridhia ombi la kusogeza mbele shughuli za uzalishaji wa madini hayo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020 hadi 2024.

Akizungumzia hoja hiyo iliyowasilishwa katika kikao hicho, Waziri Biteko alihoji uhakika wa bei ya madini hayo ifikapo mwaka 2024 katika soko la dunia na ikiwa utakuwa wakuridhisha na kuwataka kuwasilisha data zao ili ofisi yake iweze kuzifanyia kazi.

"Ni kiashira gani kinachowaonesha kuwa ifikapo 2024 kutakuwa na ongezeko la thamani kwa madini ya urani?" Biteko alihoji.

Aidha Biteko aliutaka uongozi wa kampuni hiyo kuwasilisha mchanganuo unaoonesha ongezeko la thamani ya madini ya uranium ifikapo mwaka 2024 ili wataalamu wa Wizara ya Madini wafanyie kazi na kuishauri Wizara juu ya kuridhia au kutoridhia maombi hayo.

Akizungumzia juu ya maamuzi yaliyofikiwa na kampuni hiyo, Rais wa kampuni ya Mantra Tanzania, Vasiliy Konstantinov alisema bei ya kuuza madini hayo kwenye soko la dunia imeshuka jambo ambalo litapelekea kampuni na Serikali kutokunufaika na uwekezaji huo kutokana na kuwekeza kwa hasara.

Konstantinov alisema kampuni imeamua kufika na kukaa na Wizara ya Madini ili kupata msaada na kuhakikishiwa uhakika wa kuendelea na uwekezaji huo baada ya thamani ya madini hayo kuongezeka ili kuwawezesha kuwekeza kwa faida.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa leseni na Tehama kutoka Tume ya Madini, Yahya Samamba alihoji uamuzi wa kampuni hiyo kuendelea na uwekezaji ifikapo 2024 endapo hakutokuwa na mabadiliko ya kuridhisha katika soko la dunia. 

Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mantra Tanzania, Alexander Ryabchenko alisema kwa sasa kampuni hiyo iko katika utafiti wa kutafuta njia rahisi isiyotumia gharama kubwa za uwekezaji ili kuifanya kampuni hiyo kuendelea na uzalishaji mara baada ya muda huo kufika hata kama bei ya madini hiyo haitabadilika.

Mantra Tanzania ni kampuni ya uchimbaji mkubwa wa Madini nchini yenye leseni iliyotolewa na Wizara ya Madini tangu mwaka 2013.
Tazama BMG Online TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.