LIVE STREAM ADS

Header Ads

Vikundi Manispaa ya Ilemela vyahakikishiwa mikopo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mwaka huu 2020 mikopo ya zaidi ya billioni moja kutolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.

Hayo yalibainishwa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula katika ziara ya kutembelea vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wakati akizungumza na vikundi kutoka Kata tano ikiwemo Kawekamo, Kiseke, Ilemela, Pasiansi na Nyasaka.

Alisema, milioni 600 tayari zimekopeshwa huku milioni 538 zinatarajiwa kuongezwa hivyo kufikia mwaka 2020 jumla ya bilioni 1.138 zitatolewa,zinaweza kuongezeka zaidi ya hapo kutokana na makusanyo ya mapato. 

Dkt. Mabula alisema jumla ya vikundi 671 vya halmashauri hiyo vilipatiwa elimu ya mikopo na biashara kutoka kwa ofisi ya Mbunge, ingawa changamoto iliyopo ni vikundi vingi kutokuwa na ofisi,kutorejesha kwa wakati huku alitumia fursa hiyo kufafanua umri wa kundi la vijana wanaopaswa kupata mkopo ni wale mwenye miaka 18 hadi 35. 

"Ili wanavikundi msikwame kurejesha mkopo mnatakiwa muwe na kikundi kinachofanya shughuli moja,mnaofahamiana kitabia pamoja na kutengeneza bidhaa tofauti na za vikundi vingine kwa ajili ya kupata fursa ya masoko,kuwa wabunifu katika biashara zenu huku halmashauri ikiendelea kutoa elimu ya mikopo na biashara hata kama mtu ataki kukopa halmashauri" alisema Dkt. Mabula. 
Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Ilemela Shukrani Kyando alisema Serikali ilitoa maelekezo ya fedha hizo za asilimia 10 kwa ajili ya mikopo ya wakina mama, vijana na watu wenye ulemavu kufunguliwa akaunti yake maalumu hivyo Halmashauri hiyo imetekeleza agizo hilo ambapo mpaka sasa akaunti ipo tayari na watu watarejesha na kukopa kupitia akaunti hiyo. 

Diwani wa Kata ya Kawekamo, Japhes Rwehumbiza alisema licha ya Serikali ya awamu ya tano kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa kila halmashauri kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu fedha hizo bado hazitoshi kukidhi mahitaji yao. 

"Makundi haya yanajishughulisha na ujasiriamali na kilio chao kikubwa ni fedha zinazotokana kutokidhi mahitaji yao hivyo ili kuondokana na changamoto hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri hii John Wanga anapaswa kutenga zaidi ya asilimia 10 za mapato ya ndani angalau kufikia asilimia 20 hadi 30 ili fedha hizo ziwanufaishe na kukidhi mahitaji" alisema Rwehumbiza.

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii,Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Amina Bululu aliwataka wanavikundi wa makundi hayo matatu yaliyotengewa jumla ya asilimia 10 kuhakikisha akaunti zao za vikundi kuwa hai, kupata usajili wa Manispaa, kuwa na mradi wa pamoja, kulipa ada ya kikundi, kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu. 
Imeandaliwa na Judith Ferdinand, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.