LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watoto wataka Haki zao kulindwa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Watoto mkoani Mwanza wameitaka Serikali na wadau wa watoto kuendelea kutoa elimu kwa wazazi na walezi juu ya haki za watoto ili kuhakisha wanazilinda na kufichua vitendo vya ukatili.

Kauli hiyo imetolewa Juni 16, 2021 na Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Mkoa wa Mwanza, Neema Theonest wakati akisoma risala katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika viwanja vya Furahisha mkoani Mwanza.

Akizungumzia changamoto wanazokutananazo watoto mkoani Mwanza, Neema alisema bado kunachangamoto za vitendo vya ukatili kwa watoto kwa kuwa wengi wao hawawezi kujieleza na kujikuta wakiishi katika mateso makubwa.

Alisema bado jamii haifichui vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto na uchunguzi unaonyesha wengi wao hawajui umuhimu wa kukemea vitendo hivyo ambavyo ni chanzo kikubwa cha watoto kukimbilia mtaani.

Aidha sehemu ya risala hiyo ilisema kunachangamoto kubwa ya miundombinu ya watoto wenye ulemavu katika shule nyingi za Serikali na kuomba miundombinu kuboreshwa ili kuwavutia watoto wenye ulemavu kupenda shule na kuacha utoro wakiwa katika madarasa ya awali.
Naye Meneja kutoka Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na UKIMWI (NACOPHA),Veronica Joseph ambao walishiriki katika maadhimisho hayo alisema lengo lao ni kuhakikisha watoto wanaoishi na VVU wanapata haki zao za msingi.

"Upande wetu tuanza mapema kuangalia haki ya mtoto kuishi, tunaanzia pale Mama na Baba ambao wanaishi na VVU wanapotaka kupata mtoto tunawashauri njia nzuri ya kukutana lakini pia kuhakikisha wakati wa kujifungua mama hamuambukizi mtoto hivyo tunaamini hadi kufikia 2040 hakuna mtoto atakayezaliwa akiwa na VVU" alisema Veronica.

Kwa upande wake Steven Mathias akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Ilemela,, alisema Serikali inawashukuru wadau wote wanaowahudumia watoto na kuahidi kuweka nguvu zaidi katika kutoa elimu kwa jamii juu ya kupinga ukatili kwa watoto na kuhakikisha watoto wanapatiwa haki zote za msingi.

Alisema matarajio ni Tanzania hadi kufikia 2040 kutekeleza ajenda ya Afrika ili kuhakikisha inalinda haki za watoto kama kauli mbiu inavyosema, kwa sababu Tanzania iliridhia mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za msingi za mtoto.

Takwimu zinaonyesha kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2021 jumla ya watoto 806 walikimbilia mtaani mkoani Mwanza na kati ya hao 703 walikuwa wa kiume na wakike 103 ambapo Serikali kwa kushirikiana na wadau walifanikiwa kuwarudisha nyumbani watoto 345.
Na Tonny Alphone, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.