Uchumi duni watajwa kusababisha ndoa nyingi kusambaratika
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Tonny Alphonce, Mwanza
Imeelezwa kuwa kuyumba kwa uchumi wa familia katika familia nyingi nchini ndio sababu za kuvunjika kwa ndoa nyingi na kusababisha ongezeko la Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Hayo yamesemwa na wadau wanaojihusisha na malezi ya watoto mkoani Mwanza ambapo wamewataka wazazi na walezi kuwa na mahusiano mazuri na watoto wao ili waweze kujua changamoto mbalimbali wanazozikabili hasa wanapokuwa wameingiliana na makundi mengine.
Kaimu meneja wa shirika la Railway Children Afrika la mkoani Mwanza Mary Mushi alisema wazazi wanamajukumu makubwa ya malezi na ulinzi kwa watoto hivyo wanatakiwa kutenga muda wao wa kutosha kwaajili hiyo.
Alisema miaka miwili iliyopita 2019 hadi 2021 inaonyesha mkoa wa Mwanza ulikuwa na ongezeko la watoto wa mtaani na baada ya utafiti ilionyesha watoto wengi wamekimbia makwao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo Ulevi,Wazazi kuachana,Ugomvi wa kila siku,kuyumba kwa uchumi pamoja na wazazi kukosa muda wa kuwalea watoto kutokana na majukumu waliyonayo.
“Unaweza kuona nafasi ya baba na mama kwa mtoto ni kubwa sana na wazazi hawa wanaposhindwa kutimiza wajibu wao basi hata mtoto anaweza kuharibikiwa kimaisha na kukosa mwelekeo”alisema Mary.
Alisema ili kuhakikisha tatizo la watoto kukimbilia mtaani linaisha shirika la Railway Children Afrika limekuwa likifanya jitihada za kuwaunganisha Watoto na familia zao na kisha kuwawezesha fedha za kuanzisha miradi itakayowasaidia kuendesha familia zao.
Kwa upande wake Mwanasaikolojia Bosco Bosco alisema tatizo kubwa lililopo hivi sasa ni wanandoa kushindwa kujua wapi wanaweza kupata ushauri pale migogoro ya ndoa inapoibuka na kupelekea kutafuta ushauri wa marafiki na watu wa karibu ambao wakati mwingine huwashauri vibaya na kupelekea kuachana.
Bwana Bosco alisema pamoja na dunia kubadilika kutokana na kukua kwa teknolojia nchi zilizoendelea wanasaikolojia wamekuwa msaada mkubwa katika jamii hasa katika suala zima la kutatua migogoro ya kifamilia tofauti na hapa nchini hali inayopelekea ndoa nyingi kuvunjika na kusababisha watoto kuishi katika mazingira magumu.
Wakizungumzia maadhimisho ya Siku ya Wazazi Dunia ambayo huadhimishwa tarehe mosi ya mwezi wa sita kila mwaka baadhi ya wazazi walisema ni jambo zuri mzazi kukumbushwa wajibu wake katika malezi kwa kuwa wazi wengi wamebanwa na majukumu ya kukuza uchumi wa familia na kusahau malezi.
Bwana Abdul Mshana ambae ni dereva wa daladala mkoani Mwanza amekiri wazazi kukosa muda wa malezi na mzigo mkubwa kuwaachia walimu na wafanyakazi wa ndani.
“Kutokana na mazingira ya kazi yangu mimi narudi nyumbani usiku saa 4 au saa 6 usiku nakuta watoto wamelala na mke wangu anabishara zake akitoka asubuhi hadi usiku saa moja au saa mbili kiukweli Watoto wanalelewa na dada wakazi,walimu na majirani sio vizuri lakini tafanyaje”alisema Mshana
Kwa upande wake Nancy Kitomari ambae anafanyakazi benki alisema amekuwa akitumia vema siku za mwishoni mwa wiki na siku za mapumziko kuwa karibu na watoto na kujua mahitaji yao na kutatua changamoto zao na Watoto wamekuwa na maadili mazuri.
Alisema pamoja na muda mwingi kuwa kazini lakini amekuwa akiitumia teknolojia vyema kwa kuongea na Watoto kwa njia ya simu kila anapopata nafasi ofisini na kuwaelekeza baadhi ya kazi kufanya na kuwakaza kucheza michezo ya hatari na wamekuwa wakimwelewa.
Tarehe 1 Juni ya kila mwaka ni maadhimisho ya wiki ya Kimataifa ya wazazi iliyowekwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2012.
Siku ya wazazi ilianzishwa kama fursa ya kupongeza wazazi wote duniani kote na kuwashukuru kwa ajili ya jitihada zao za malezi mbele ya watoto wao.
No comments: