LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wazazi Sindiga walia na adha ya maji "watoto wanakosa masomo"

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Wananchi wa Vitongoji vya Mbambazi na Tatazi vilivyopo Kijiji cha Mkidu mkoani Singida wameiomba Serikali kuwapelekea huduma ya maji safi na salama ili kuwapunguzia wazazi na watoto wao umbali mrefu wa kusaka maji.

Akizungumza kwa niaba ya wanavijiji wenzake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkidu, Brayton Nazael alisema tatizo la maji katika Kijiji hicho ni la muda mrefu na hakuna dalili zozote za kupatiwa maji kutoka serikalini au kutoka kwa wafadhili.

Nazaeli alisema Vitongoji vyote vya Katazi na Mbabazi vimekuwa na shida ya maji kwa muda mrefu hali inayopelekea binadamu kuchangia maji ya Mto mdogo uliopo na mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi na kondoo hali ambayo ni hatari kwa afya za wanakijiji hao.

"Kwa kweli maji haya yaliyopo siyo salama kwa sababu ukiyaangalia vizuri yana vijidudu ambavyo vinaonekana kwa macho lakini hakuna namna wananchi wanayatumia hivyo hivyo lakini wengi wanaishia kuugua magonjwa mbalimbali" alisema Nazaeli.
Nao baadhi ya watoto wanaosoma darasa la awali Shule ya Msingi Tatazi ambao walikutwa wakisaka maji walisema wamekuwa wakiwasaidia wazazi wao kuchota maji asubuhi kabla ya kwenda shule na jioni mara baada ya kurudi kutoka Shule kwa kuwa maji ni ya shida katika Kijiji chao.

Naye Warda Francis ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mbabazi alisema wanaishi maisha ya tabu kutokana na ukosefu wa maji na watoto wa kuanzia umri wa miaka mitatu na kuendelea nao wamekuwa wakitumika kwenda kuchota maji ili kusaidia angalau nyumbani kupatikane maji ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya familia.

"Kuna wakati watoto wanachelewa kwenda Shule kutokana na kuchelewa kupata maji kutoka kwenye chemchem maana wakati mwingie unasubiria hadi yajae ndio uchote sasa kama unavyojua watoto wanamichezo mingi wakati mwingine wanaanza kucheza huku wakisubiri maji kujaa na matokeo yake wanachelewa au hawaendi tena shule kabisa" alieleza mama huyo.
Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la Maranatha, Deo Rugaba ambaye anatoa huduma pia katika maeneo mbalimbali ya Vijiji vya Singida alisema aliliona tatizo la maji mkoani humo na kuanza utaratibu wa kuwajengea visima vya maji ya kuvuta na mashine maarufu kama visima vya mdundiko.

Alisema pamoja na kuanza ujenzi wa visima hivyo kwa baadhi ya Vijiji, changamoto aliyonayo ni vifaa duni vya kuchimbia visima virefu lakini pia gharama ya kuweza kuchimba kisima kimoja ni kubwa ambapo hufikia hadi milioni 12 kwa kisima kimoja.

"Hali ya maji sio nzuri hasa upande wa akina mama na watoto muda mwingi wanautumia kutafuta maji, mimi natamani nipate nguvu ili kuhakikisha kila Kijiji kinapata angalau visima viwili ili waache kuchangia maji na mifugo maana ni hatari japo wao wanasema wamezoea" alisema Mchungaji Deo.
Mkoa wa Singida ni miongoni mwa Mikoa yenye changamoto ya maji ambapo tangu mwaka 2017 tafiti na uchimbaji wa visima umekuwa ukiendelea kwa baadhi ya Vijiji vikiwemo Unyambwa, Kisasida na Unyamikumbi.
Na Tonny Alphonce, Singida

No comments:

Powered by Blogger.