LIVE STREAM ADS

Header Ads

TAMWA yaendesha Mdahalo kwa Waandishi wa Habari mkoani Morogoro

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimeendesha mdahalo kwa waandishi wa Habari mkoani Morogoro kwa lengo la kujadili hali halisi ya ukatili wa kingono katika vyombo vya habari na kuweka mikakati ya kuvitokomeza.

Mdahalo huo uliobeba dhima kuhusu vitendo vya ukatili wa kingono ndani ya vyombo vya habari umefanyika Julai 22, 2021 mjini Morogoro na kuwajumuisha pia wawakilishi wa vyombo mbalimbali vya habari kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Dar es salaam na Mwanza.

Mkurugenzi Msaidizi wa TAMWA, Sylivia Daulinge amebainisha kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa ndani ya vyombo vya habari kuna ukatili na unyanyasi wa kingono hususani kwa wanawake lakini waandishi wa habari hawaripoti matukio hayo na badala yale huripoti yale yaliyo nje ya vyombo vyao.

Amesema mdahalo huo utasaidia waandishi wa habari kupeana mikakati na mbinu mbalimbali za kupambana na ukatili na unyanyasi wa kingono katika vyombo vya habari hususani kusaidia kuleta mabadiliko ya kisera yatakayotambua nafasi ya mwandishi wa habari mwanamke.

Naye Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Morogoro (MOROPC), Lilian Kasenene amesema mdahalo huo umekuwa na manufaa makubwa na utawasaidia wanahabari kutonyamazia vitendo vya unyanyasi na ukatili wa kingono katika ofisi zao.

Akiendesha mdahalo huo, Afisa Programu kutoka TAMWA, John Ambrose alianisha makundi ya wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri, Serikali na taasisi zake, wadau wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari na washiriki kueleza ni namna gani makundi hayo yanashiriki kuzuia ama kutenda ukatili wa kingono ambapo wahariri na wamiliki ndilo kundi lililoonekana hatari zaidi kujihusisha na rushwa ya ngono.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Afisa Programu kutoka TAMWA, John Ambrose akiendesha mdahalo huo.
Mkurugenzi Msaidizi wa TAMWA, Sylivia Daulinge akikagua mapendekezo yaliyotolewa na washiriki kwenye mdahalo huo ambayo yakitekelezwa yatasaidia kupambana na ukatili wa kingono katika vyombo vya habari.
Katibu wa MOROPC, Lilian Kasenene ameishukuru TAMWA kwa kuandaa mdahalo huo akisema utaleta chachu kwa waandishi wa habari kutonyamazia vitendo vya unyanyasi wa kingono katika vyombo vya habari.
Washiriki wakiandika mapendekezo mbalimbali yatakayosaidia kuweka mikakati ya kupambana na ukatili wa kingono katika vyombo vya habari.
Washiriki wa mdahao huo wakiwa kwenye picha ya pamoja.

No comments:

Powered by Blogger.