LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Gwajima azindua Mwongozo wa ajira za muda kwa wahitimu wa kada za Afya

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Na Atley Kuni- Dodoma
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo nchini imekamilisha mwongozo wa kitaifa wa kuwawezesha wahitimu wa kada za afya ambao hawana ajira rasmi ili waweze kuajiriwa kwa muda.

Hayo yalisemwa Septemba 15, 2021 na Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri mjini Dodoma.

Dkt. Gwajima alisema, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau wamekamilisha mwongozo wa Kitaifa wa Kujitolea (National Health Workforce Volunteerism Guideline) unaotoa utaratibu wa namna bora ya Hospitali na Vituo vya afya kutumia wahitimu wa kada ya afya ambao hawajaajiriwa ili waweze kutumika rasmi katika utoaji wa huduma za afya kwa njia ya kujitolea.

“Mwongozo huo ni mkakati mahususi wa kuboresha huduma za afya kwa kukabiliana na uhaba wa watumishi katika sekta ya Afya nchini hii hapa ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa upatikanaji na utoaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi” alisema Waziri Gwajima.

Waziri Gwajima alisema, Serikali ya awamu ya sita inaendelea kutekeleza Afua za Sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na kuajiri watumishi 2,726 wa kada za Afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, lengo likiwa ni kuikamilisha utoaji wa huduma za afya nchini.

Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima alisema Mkutano huo ambao umebebwa na kaulimbiu isemayo Ustahimilivu wa Mifumo ya Afya katika Mapambano dhidi ya UVIKO-19; ‘changamoto na fursa’ unatoa ishara ni kwa namna gani wataalam wa afya wanavyoshirikiana kutekeleza majukumu yao wanapo kabiliana na ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (UVIKO -19) tokea ulipoingia hapa nchini.

“Pamoja na changamoto zilizopo, mmeendelea kujitoa na kutumia weledi wenu katika kuihudumia jamii, hili ni jambo la kizalendo, hongereni sana, nichukue nafasi hii kuwaelekeza viongozi wote wa ngazi zote kushiriki kuwahamasisha wananchi kwenda kupata chanjo ya UVIKO -19 kwani chanjo hizo ni Salama" alisisitiza Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange alisema Serikali kuanzia awamu ya tano na ya sita zimekuwa zikitoa kipaumbele katika huduma za fya, ambapo katika mwaka fedha wa 2021/22, jumla ya Hospitali 28 zinakwenda kuanza ujenzi wa Hospitali za Wilaya ambazo hazikuwepo kabisa, aidha Tarafa zote 207 zitajengewa Vituo vya afya huku Tarafa 150 zikiwa tayari zimeshapelekewa fedha katika mwanzo wa mwaka kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Dkt. Dugange aliwakumbusha Waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri, kusimamia ipasavyo rasilimali zote zinazofika kwenye maeneo yao huku akiwataka kutumia Mkutano huo kama sehemu ya darasa la kujifunza katika kukabiliana na Uviko-19 kwa kubadilisha uzoefu kutokana na changamoto kutofautiana.

Akitoa salaam za Wizara ya Afya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi alihimiza suala la uimarishaji wa utoaji wa huduma kwani Pamoja na kujenga miundombinu lakini saula la msingi ni uimarishaji wa utoaji huduma za afya, amesema watoa huduma lazima wawe na lugha zisizo za kumkera mtu anayepatiwa huduma.

Naye Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe aliwataka Waganga wakuu wa Mikoa kuwa mstari wa mbele katika suala la kuchanja, aidha Wizara itafatilia kujua Mkoa na Halmashauri kinara katika zoezi la kuchanja chanjo ya Uviko-19.

Mapema akiongea katika Mkutano huo, Dkt. Florence Temu, kutoka AMREF na mwakilisi wa Non state Actors aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudu kubwa zinazo chukuliwa katika mapambano dhidi ya Uviko-19, na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali.

“Awali kulikuwa na vituo vya kutolea huduma za chanjo 500 lakini kwa takwimu za sasa inaonesha idadi ya vituo hivyo imeongezeka na kufikia 1500, hii ni hatua kubwa, tunaimani Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau lakini pia kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa za Uviko-19" alisema Dkt. Florence.
Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima, wakati akizindua Mwongozo ulioandaliwa na Serikali kwa ushirikiano na wadau kwa ajili ya ajira za muda kwa wahitimu wa kada ya Afya.

No comments:

Powered by Blogger.