LIVE STREAM ADS

Header Ads

Vigogo NHIF wapandishwa kizimbani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com 
Na Shomari Binda, Musoma
Aliyekuwa Meneja Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Taifa (NHIF) Mkoa wa Mara, Mgude Bachunya (51) na wenzake wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka kutokana na tuhuma za makosa mbalimbali ikiwemo uhujumu uchumi na kuisababishia NHIF hasara ya zaidi ya Shilingi Bilioni 3.38.

Mgude amefikishwa mahakamani na watuhumiwa wengine ambao ni aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa NHIF Mkoa Mara, Francis Mchaki (37) pamoja na aliyekuwa Msimamizi wa Mfuko huo Mkoa Mara, Dkt. Leonard Mitti (51).

Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda makosa mbalimbali kwa nyakati tofauti kati ya Januari 2013 hadi Machi 2016 ambapo Bachunya anakabiliwa na makosa 20, Mchaki makosa 37 na Mitti makosa 11 ambapo wamesomewa mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Mara.

Wakili wa Serikali, Tawabu Issa ameeleza mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Eugenia Rujwahuka kuwa miongoni mwa makosa wanayoshtakiwa nayo mbali na kosa la uhujumu uchumi ni pamoja na matumizi mabaya ya ofisi na matumizi mabaya ya madaraka huku wakiwa ni watumishi wa umma.

Makosa mengine ni kuusababishia hasara mfuko wa NHIF, kugushi nyaraka mbalimbali kwa lengo la kumdanganya mwajiri, kutumia nyaraka za uongo pamoja na ufujaji wa pesa za umma. Imeelezwa kuwa uchunguzi unaendelea ili kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wengine wanaohusika katika tuhuma hizo.

Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Rujwahuka amesema Mahakama hiyo haina mamalaka kisheria kusikiliza kesi hiyo na hivyo kuamuru watuhumiwa hao kupelekwa mahabusu huku taratibu zikifanyika kati ya taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashataka kwa hatua zaidi za kisheria.

"Ingawa dhamana iko wazi lakini Mahakama hii kama nilivyoeleza hapo awali haina mamlaka ya kutoa dhamana hivyo mtapelekwa rumande lakini mnaweza kuanza mchakato wa kuomba dhamana kupitia Mahakama Kuu muda wowote na mkitimiza masharti mtapewa hiyo dhamana, kwa sasa mnapelekwa mahabusu hadi Novemba 15 mwaka huu kesi hii itakapoletwa tena hapa" ameeleza Hakimu Rujwahuka.

No comments:

Powered by Blogger.