LIVE STREAM ADS

Header Ads

Tanzania na Burundi kuongeza ushirikiano kukuza Sekta ya Posta

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari akizungumza na ujumbe wa Maafisa Waandamizi kutoka Shirika la Posta Burundi wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Posta Burundi, Lea Ngabire walipotembelea Mamlaka hiyo kwa ziara ya mafunzo.
***

Shirika la Posta la nchini Burundi limeweka bayana dhamira yake ya kushirikiana na Tanzania katika kukuzasekta ya Posta nchini humo ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi zaidi katika usimamizi wa masuala ya Posta.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya posta wa Burundi, Lea Ngabire alipozuru Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) akiambatana na ujumbe wa Maafisa Waandamizi wa Posta Burundi katika ziara ya mafunzo.

“Tumefikahapa TCRA na kujionea shughuli mbalimbali za mawasiliano na lengo letu ni kuona namna nchizetu mbili zinavyowezakushirikiana katika kukuza na kuendelezasekta ya posta” alibainisha Ngabire.

Ujumbe wa Maafisa hao umejumuisha Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Posta Burundi, Nyayishimiye Olivier na Mkuu wa masuala ya Barua, Misirakuba Deo.

Akipokea ujumbe huo Jumatano Tarehe 17 Novemba 2021, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari aliwakaribisha na kuwaeleza kuwa TCRA kama mdhibiti wa sekta ya Mawasiliano nchini Tanzania inatambua umuhimu wa ushirikiano wa mawasiliano hasa kikandana imekuwa mshirika muhimu wa mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Lengo letu ni kuhakikisha sekta ya mawasiliano nchini Tanzania inasimamiwa kwa uthabiti na kwa upande wa posta TCRA imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali za kikanda na kimataifa na kama mnavyofahamu pia Makao Makuu ya Posta Afrika yapo hapa nchini” alibainisha Jabiri.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Posta Burundi, Lea Ngabire akisaini kitabu cha wageni wakati alipotembelea Makumbusho ya Mawasiliano iliyopo Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Katika ziara hiyo ya mafunzo, Ngabire aliambatana na MaafisaWaandamizi wa Posta Burundi.

Pia Mkurugenzi Mkuu Jabiri aliwaeleza wajumbe hao kwamba Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha sekta ya mawasiliano barani Afrika inaimarika na ndiyo sababu imekuwa ikishirikiana na Shirika la Posta Afrika (PAPU) kuhakikisha ujenzi wa Ofisi ya PAPU makao makuu ambayo ujenzi wake unaendelea jijini Arusha unakamilika kwa wakati ifikapo 2022.

Naye Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa TCRA, Dkt. Emmanuel Manasseh ambaye sekta ya Posta inasimamiwa na kurugenzi anayoingoza alibainisha kwamba hakuna namna uchumi wa kisasa utajengwa bila kuhusisha posta kwani sekta hiyo ni muhimu katika masuala ya usafirishaji na ufikishaji wa taarifa mbalimbali zinazowezesha kujenga uchumi wa kisasa (Uchumi wa Kidijitali).

“Tunapoenda kwenye uchumi wa kidijitali posta ni sekta muhimu sana ambayo hatuwezi kukwepa kuitumia kwani itatuwezesha kufikia azma ya kujenga uchumi wa kidijitali” Alisisitiza Dkt. Manasseh.

Mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo ujumbe huo ulibainisha kufurahishwa na maarifa waliyopata baada ya kutembelea TCRA ili kujifunza na kuahidi kwamba watatendea kazi yale waliyojifunza katika kukuza sekta ya Posta nchini Burundi.
Na Mwandishi Maalum, Dar

No comments:

Powered by Blogger.