LIVE STREAM ADS

Header Ads

Viongozi wa CCM Nyamagana waibukia TANESCO, tatizo umeme

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Mwanza limetaja mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha mvua chache kuwa sababu kubwa ya uwepo wa upungufu wa umeme uliopo.

Kufuatia changamoto hiyo, shirika hilo limewataka wateja wake kuwa wavumilivu kwani linaendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kukabiliana nayo huku likibainisha kwamba itakwisha baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa umeme wa bwawa la Julius Nyerere unaotarajiwa kukamilika Juni 2024 kwani utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2115 ambazo zitakidhi kabisa mahitaji ya Taifa.

Hayo yalibainishwa Oktoba 27, 2022 na Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mwanza Mhandisi Abdallah Mitenda kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyamagana waliofika ofisini kwake wakiongozwa na Mwenyekiti wao Peter Begga lengo likiwa ni kujua sababu ya uwepo wa mgawo wa umeme kwa wananchi ambao wamekuwa wakiwasumbua mara kwa mara.

Mhandisi Mitenda alisema vituo vya uzalishaji umeme havijazidiwa kwani vina uwezo mkubwa wa kuhudumia wananchi lakini changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni kushuka kwa kiwango cha maji kwenye vituo vya Kihansi, Mtela na Kidatu hali iliyosababishwa na upungufu wa mvua hivyo kupungua kwa kiwango cha umeme unaozalishwa.

“Kiwango cha maji kikishuka uzalishaji wa umeme unapungua na ukipungua unaathiri demand (mahitaji) ya watumiaji na hii ni kwa nchi nzima maana hivi vituo vikubwa vya maji vikizalisha umeme vinaingiza kwenye gridi ya taifa.

“TANESCO tunaendelea kufanya mikakati mbalimbali ikiwemo kuongeza mashine ambazo zinategemea maji ili kufanya kazi hadi sasa kuna mashine moja tumeifunga pale Kinyerezi inafanyiwa majaribio Novemba 2022 itaingizwa kwenye gridi ya megawati 70 itapunguza upungufu uliopo kwenye vituo vya maji, mashine hiyo inafika megawati 130 hadi 170 kwa siku itagawanywa kwenye mikoa yote” alieleza Mitenda ambaye pia ni Mhandisi Mkuu wa Tanesco Mkoa wa Mwanza.

Naye Kaimu Afisa Masoko wa TANESCO Mkoa wa Mwanza, Prisca Kayaga aliwaomba wateja wao kuwa wavumilivu kwani wana matumaini na uwekezaji unaofanywa na Serikali ambao unawapa mwanga mzuri mbeleni kutokana na miradi mikubwa inayotekelezwa.

“Kwa mfano mradi wa Julius Nyerere ambao ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalishga mega wati 1215 ambazo zikiingizwa kwenye gridi ya taifa zina uwezo wa kutupatia umeme hadi wa ziada, tunazidi kuwaomba sana wananchi na wateja wetu watuvumilie lengo la Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kutatua changamoto za wananchi na sisi tupo kwa ajili ya kumsaidia” alisema Kayaga.

Baada ya kupata maelezo hayo kutoka kwa wataalamu hao wa masuala ya nishati, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana Peter Begga akalishauri shirika hilo kutoa taarifa mapema kwa wananchi kuhusu kukatika kwa umeme ili wajiandae maana wapo ambao wanategemea umeme kwa ajili ya kufanya biashara ambazo ndiyo zinazowaingizia kipato.

“Lengo la ujio wetu hapa ni kupata majawabu ya kukatika umeme mara kwa mara, malalamiko yanakuja kwenye chama na sisi kama chama ambacho tunaongoza nchi tuliona lazima tujiridhishe ili tuwe na majibu sahihi kwa wananchi watakapotuuliza” alisema.

“Lakini ni vizuri muwe mnawapa taarifa mapema wananchi kuhusu kukatika kwa umeme naamini TANESCO ni biashara na kwenye biashara Customer Care (Huduma kwa Mteja) taarifa ni kitu muhimu sana kwa mteja” alisema Begga na kuongeza;

“Umeme na maji kwa sasa mimi navichukulia kama ni mojawapo ya haki za binadamu maana unakuta mtu ameishanunua luku kwa ajili ya matumizi yake,  wengine kwa ajili ya matumizi ya kiuchumi hivyo ana haki ya kupata taarifa ya kukosekana kwa huduma hiyo mapema” alishauri Begga.

Viongozi walioambatana na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana Peter Begga ni pamoja na Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana Geofrey Kavenda, Mwenyekiti wa UWT Nyamagana Witness Makale, Katibu UWT Nyamagana Getrude Mboyi na Katibu UVCCM Nyamagana Ramadhan Omary.
Imeandaliwa na Clara Matimo, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.