LIVE STREAM ADS

Header Ads

Makamanda wa Chuo cha Kijeshi Duluti wafanya ziara Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkoa wa Mwanza umepokea ugeni wa maafisa wa kijeshi kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu kilichopo Duluti mkoani Arusha ikiwa ni ziara ya mafunzo.

Akizungumza Oktoba 10, 2022 kwenye kikao cha mapokezi ya maafisa hao, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima alisema maafisa hao watatembelea na kukagua miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa mkoani Mwanza. 

Alisema Mkoa wa Mwanza una fursa mbalimbali za kiuchumi ambapo suala la ulinzi na usalama ni la msingi katika kuimarisha amani na utulivu hivyo ujio wa maafisa hao utasaidia kuchochea utendaji kazi wenye tija.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Duluti, Brigadia Jenerali Sylvester Ghuliku alisema ziara hiyo pia itatumika kufanya utafiti juu ya amani na usalama kwa maendeleo ya taifa.

"Tumechagua kuja Mwanza kutokana na Mji huu kukua kwa kasi na una mahusiano ya karibu na nchi zinazotuzunguka Africa Mashariki hivyo tunaamini changamoto za ulinzi na usalama haziwezi kukosekana na ndiyo maana tumekuja kujifunza nakushauriana namna ya kuzitatua kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu" alieleza Brigadia Jenerali Ghuliku.

Alisema jukumu la Chuo hicho ni kuwaandaa maafisa wakuu ili waweze kufanya kazi katika ngazi za juu katika majeshi yao.

Maafisa hao walitembelea mradi wa reli ya kisasa (SGR)eneo la Fela, daraja la Kigongo-Busisi, stendi ya kisasa ya mabasi Nyegezi na mradi wa Soko Kuu Mwanza.

Nao baadhi ya maafisa walisema kutokana na ziara hiyo ya kimasomo, watajifunza mahusiano ya ndani yatakayowawezesha kujua utendaji kazi katika maeneo mbalimbali hatua itakayowasaidia kutimiza vyema majukumu yao ya kiusalama.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akizungumza kwenye kikao cha mapokezi ya maafisa wakuu kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Duluti Arusha.
Maafisa wa kijeshi kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Duluti Arusha.
Maafisa wa kijeshi kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Duluti Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima (kushoto) akiwa na Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Duluti Arusha, Brigadia Jenerali Sylvester Ghuliku (kulia).

No comments:

Powered by Blogger.