LIVE STREAM ADS

Header Ads

Tani Milioni 1.4 za Makaa ya Mawe zasafirishwa nje ya nchi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Ephrahim Mushi amesema kuwa tangu kuanza kusafirishwa kwa makaa ya mawe mapema Oktoba 2021, hadi Januari 2023 jumla ya tani milioni 1.14 za makaa ya mawe yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 201.27 zilisafirishwa nje ya nchi kupitia Bandari ya Mtwara na kuwezesha Serikali kukusanya maduhuli ambayo yamechangia kwa kiwango kikubwa katika makusanyo ya Sekta ya Madini katika mkoa wa Mtwara.
 
Mhandisi Mushi aliyasema hayo leo tarehe 23 Januari, 2023 mkoani Mtwara kwenye mahojiano maalum ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kipindi maalum chenye lengo la kuangalia mchango wa Sekta ya Madini katika kuwawezesha watanzania kiuchumi pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii katika mikoa ya Njombe, Ruvuma na Mtwara.

Alisema kuwa kupitia usafirishaji wa makaa ya mawe kwenda nje ya nchi kupitia Bandari ya Mtwara, Serikali kupitia Tume ya Madini ilikusanya maduhuli ikiwa ni pamoja na marabaha Dola za Marekani milioni 6.038, ada za ukaguzi Dola za Marekani milioni 2.012 na vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi Dola za Marekani, 3100.
 
Aliongeza kuwa kiasi cha tani 30 za makaa ya mawe zilisafirishwa kwenda Zanzibar na kusisitiza kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kuna tani zaidi ya 200,000 za makaa ya mawe ambayo yamehifadhiwa katika maeneo mbalimbali ambazo zinasubiri kusafirishwa nje ya nchi.

Aliongeza kuwa kampuni zinazohusika na usafirishaji wa makaa ya mawe nje  ya nchi ni pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Ruvuma Coal Limited, Jitegemee Holding Company Limited, Gold Walk Limited, SEBDO na Aria Commodities International Limited.

Aliendelea kusema kuwa makaa ya mawe yamekuwa yakisafirishwa katika nchi za India, Senegal, Ufaransa, Misri, Poland, Zanzibar, Ghana, Kenya, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Netherland huku Ofisi  ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara ikisimamia zoezi la upakiaji wa makaa ya mawe kwenye meli kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali.
 
Akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Mushi alisema kuwa awali ofisi yake ilipangiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 4.279 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo kutokana na ofisi hiyo kuendelea kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa maduhuli baadaye lengo liliongezwa hadi shilingi bilioni 5.253 kwa kipindi husika ikiwa ni nyongeza ya asilimia 22.77.

Alifafanua kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 2022 hadi Januari, 2023 ofisi yake imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 4.556 ikiwa ni lengo la asilimia 86.7 ya lengo la makusanyo lililowekwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023.
 
“Tumeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya ukusanyaji wa maduhuli ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na kuongeza kasi ya utoaji wa leseni za madini, ambapo hadi kufikia kipindi cha mwezi Juni, 2023 ninamini lengo litakuwa limevukwa,”alisema Mhandisi Mushi.

Wakati huohuo wakizungumza kwa nyakati tofauti watumiaji wa makaa ya mawe na wasafirishaji sambamba na kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya usimamizi wa Sekta ya Madini walisema kuwa manufaa makubwa ya makaa ya mawe yenye ubora wa hali ya juu yameendelea kuonekana.
 
Akizungumza kwenye mahojiano maalum, Msimamizi wa Sehemu ya Kuhifadhi Makaa ya Mawe inayomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)-Mtwara, Andrea Tela alisema kuwa shirika hilo linachimba makaa ya mawe katika mgodi wake uliopo Kiwira mkoani Mbeya ambapo lipo katika mpango wa kuiuzia kampuni ya Uswisi ( _Swiss Firm_ ) tani 60,000 za makaa ya mawe kwa mwezi.

Aliendelea kusisitiza kuwa STAMICO imejipanga kutanua soko lake ambapo kwa siku za mbeleni ina mpango wa kuendelea kuuza tani nyingi zaidi za makaa ya mawe kwa nchi mbalimbali duniani kulingana na mahitaji ya soko.

Naye Mhandisi Uchenjuaji wa Madini kutoka Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara, Mhandisi Victor Kamuhabwa aliongeza kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikipokea makaa ya mawe tani 300 hadi 1300 kutoka Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma kwa siku na kuongeza kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikitumia kati ya tani 400 hadi 600 kwa siku kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa saruji na kuzalisha umeme pale panapotokea mahitaji makubwa ya umeme.

No comments:

Powered by Blogger.