LIVE STREAM ADS

Header Ads

Polisi kuwashughulikia madereva, makondakta wakorofi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Jeshi la Polisi limewaonya madereva daladala wanaokiuka sheria za usalama barabarani na kuapa kuwachukulia hatua kali za kinidhamu.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Viginia Sodoka aliyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa madereva, makondakta na wapiga debe wa daladala jijini Mwanza.

Sodoka alisema baadhi ya madereva daladala jijini Mwanza wanalalamikiwa kukatisha safari (route) kwa baadhi ya maeneo ikiwemo Kisesa, Nyashishi na Usagala hivyo msako wa kuwabaini unaendelea ili kuwashughulikia.

Pia Sodoka alionya tabia ya baadhi ya makondakta kuwazuia wanafunzi kupanda daladala na kuwasababishia adha kubwa hususani nyakati za asubuhi na jioni akisema nao wataanza kushughulikiwa na jeshi hilo.

Ili kudhibiti uhalifu, Sodoka aliwataka madereva na makondakta kuhakikisha wanatoa taarifa kwa polisi wanapomshuku abiria yeyote ama wanapoona mzigo wanaoutilia mashaka ikiwemo dawa za kulevya kama bangi ama nyara za Serikali.

"Ukimuona abiria ambaye humwelewi, amebebeba mzigo ambao unautilia mashaka mfano bangi ama nyara za Serikali, unapaswa kufikisha gari Kituo cha polisi vingineno akikamatwa, dereva na kondakta wote mnakamatwa pia" alisema Sodoka.

Sodoka pia aliwakumbusha madereva kutambua kwamba familia zinawategemea hivyo wanapokuwa kwenye vyombo vya usafiri wazingatie sheria, waepuke mwendo kasi, ulevi na kuhakikisha wanakuwa na lugha nzuri kwa abiria huku wakizingatia mavazi nadhaifu wakiwa kazini.

Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Nyamagana, Peter Mizambwa alisema; "tutaendesha oparesheni na watakaokamatwa kwa makosa mbalimbali tutawafikisha mahakamani. Lazima tuhakikishe madereva na makondakta wanafuata sheria na kanuni zilizowekwa".

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Daladala Mkoa Mwanza (MWAREDDA), Mjarifu Manyasi aliahidi kushirikiana na jeshi la polisi ili kukabiliana na changamoto za usafirishaji ikiwemo kukatisha safari, kuzuia wanafunzi kupanda daladala pamoja na wizi ambao umekuwa ukiwasibu baadhi ya abiria katika vituo vya daladala.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Chama cha Makondakta na Wapiga Debe Mkoa Mwanza (UVDS), Mlimi Juma alisema watahakikisha wanakuwa mabalozi wa usalama barabarani, abiria hawasumbuliwi katika vituo vya daladala, kudhibiti uhalifu ikiwemo wizi huku akiomba jeshi la polisi kuwachukulia hatua kali baadhi ya askari wasio waadilifu wanaoshirikiana na wahalifu.
#BMGHabari

No comments:

Powered by Blogger.