LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali yahimizwa kuanzisha Shule za Awali visiwani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali imeombwa kuanzisha madarasa ya awali katika visiwa vidogo vilivyoko katika Ziwa Victoria ili kuwaondolea hatari ya kuzama maji watoto wanapo safiri na mitumbwi kufuata shule zilizopo katika visiwa vikubwa vyenye sifa ya kuwa na shule za misingi.

Kauli hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na wadau wa maendeleo na watoto walipokuwa wakichangia mada katika kikao cha wadau wa masuala ya ukatili dhidi ya watoto kilichofanyika jijini Mwanza na kuongozwa na mwenyekiti wa uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali Bibi Mwantumu Mahiza.

Juvenary Matagili ambae ni mdau wa uvuvi amesema watoto wengi wanaopatikana katika visiwa vidogo ambavyo havina sifa ya kuwa na shule wengi wanakosa haki yao ya msingi ya kupata elimu kutokana na utaratibu huo wa visiwa vidogo kutojengwa shule.

Matagili ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuanziasha angalau madarasa ya awali katika visiwa hivyo vidogo ili watoto wapate nafasi ya kufundishwa na watapofikia hatua ya kuingia darasa la kwanza tayari watakuwa na uelewa wa kuweza hata kujilinda watakapoanza kupanda mitumbwi kwa ajili ya kwenda shule kwenye visiwa vyenye shule.

‘Watoto wanaovuka kwenda ng’ambo wapo hatarini kuzama kwa kuwa wanavuka kwa kutumia boti za mbao ambazo hupasuka wakati wowote na kuzama na wakati wa mvua madaftali ya watoto yanalowana na wengine wanashindwa kabisa kwenda shule na wakati wa kurudi shule wanarudi usiku inategemea na muda Boti itakapoanza safari ya kurudi kisiwani’ alisema Matagili.
Naye Mkurugenzi wa shirika la Thamani ya Mwanamke Tanzania, Nyamui Lumambo amezitaja sababu zingine za ongezeko la watoto wa mtaani zinachangiwa mikopo holela inayochukuliwa na wanawake ambao hujikuta wanaingia kwenye madeni makubwa na kusahau kulea watoto na matokeo yake watoto hukimbilia mtaani.

‘Kutokana madeni kuongezeka kwenye familia kuna wazazi wanawatumia watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi mitano kuomba pesa kwa wapita njia, hii tabia ipo Mwanza wazazi wanajificha na kuwatuma watoto kuomba pesa kwa kila mpita njia na kiuhalisia watoto hao walitakiwa kuwa shule’ alisema Nyamui.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Uratibu wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Bibi Mwantumu Mahiza ameyataka mashirika 578 yanayotoa huduma jijini Mwanza kuungana ili kutatua changamoto mbalimbali zinazo wakabili watoto wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Mwanza.

Bibi Mwantumu amesema jiji la Mwanza linamashirika mengi ya kusaidia watoto zaidi ya 200 lakini inasikitisha kuona bado kuna wimbi kubwa la watoto wanaofanyiwa ukatili na ambao wanaoishi katika mazingira hatarishi hadi hivi sasa.

‘Madhara wanayopata watoto ni makubwa kuliko tunavyofikiri,kuna wengine wanasema kuna watoto hawapendi kurudi kwa wazazi wao,nani hapendi amani katika dunia hii? lazima tukubaliane tuna kila sababu ya kutafuta njia ya kuwasaidia watoto hawa na ikiwezekana hata kwa kila mmoja wetu kuchukua mtoto mmoja na kumlea’ alisema Bibi Mwantumu.

Mwanza, jiji la pili kwa ukubwa nchini Tanzania, lina idadi ya watoto wa mitaani inayoonekana kuongezeka kila siku zinavyokwenda.

Utafiti uliofanyika mwaka 2008 na Shirika la Consortium Street Children uligusa watoto na vijana 443 huku wengi wao wakiwa (88.7%) wakiwa ni watoto wa mitaani wa kutwa; 11.3% iliyobaki hurudi nyumbani usiku.

Utafiti uliofanywa huo ulijumuisha watoto na vijana wa umri mbalimbali huku wanaume wengi zaidi (411) kuliko wanawake (32) wakishiriki katika utafiti huo.
Na Tonny Alphonce, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.