LIVE STREAM ADS

Header Ads

DC Ilemela: Usalama wa mtoto uko mikononi mwa jamii

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa wilaya Ilemela.
***

Na Tonny Alphonce, Mwanza
Imeelezwa kuwa kama jamii itakuwa tayari kusimamia malezi kwa watoto na kutoa ulinzi wa karibu vitendo vya ukatili na unyanyasaji vitapungua katika jamii.

Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Masala wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika kata ya Kitangiri ambapo amewataka wazazi,walezi,walimu na viongozi wa dini wahakikishe wanaripoti na kudhibiti vitendo viovu wanavyofanyiwa watoto wadogo ili kulinda vizazi vya taifa lijalo.

“Matukio ya ubakaji,ulawiti na mauaji kwa watoto yanaongezeka siku hadi siku sasa tukiamua kukaa kimya na kuacha kukemea tutaharibu taifa na ndoto za watoto wetu zitapotea”.Alisema Mhe Masala.

Mhe Masala ameitaka pia jamii kuacha kuchagua aina ya matukio ya kuripoti na aina ya watoto wa kuwasaidia kwa kuwa watoto wote ni sawa nani mali ya jamii.

Kwa upande wake katibu tawala wa wilaya ya Ilemela ndugu Said Kitinga amewataka wananchi kutumia ofisi yake kwaajili ya kuwasilisha changamoto mbalimbali wanazozipata ikiwemo kunyimwa haki pindi wanapofatilia haki za watoto waliotendewa vitendo vinavyo hatarisha maisha yao.

“Ofisi yangu ipo wazi kwa changamoto zote mlizonazo wananchi likiwemo hili la usalama wa watoto mnaweza kutoa taarifa mapema hata pale mnapoona mtoto fulani yupo kwenye hatari ili asaidiwe mapema,tunao maafisa ustawi wa jamii wanashughulika na mambo hayo”.alisema Kitinga.

Wakati huo huo daktari Samson Marwa ambae ni mganga mkuu wa wilaya ya Ilemela amewaasa wananchi kuhakikisha watoto wanacheza katika maeneo yenye usalama hasa kipindi hiki cha mvua ili wasipate ugonjwa wa kipindupindu na kusisitiza watoto na mabinti wapatiwe chanjo ya Surua Rubela.

Naye Vicenti Malinyo mkazi wa Bwiru ameitaka serikali kupitia jeshi la Polisi na Mahakama kuhakikisha watuhumiwa wote wa matukio ya ukatili na unanyanyasaji wanahukumiwa kulingana na sheria za nchi zinavyoelekeza na kuacha tabia ya kuchukua rushwa na kuwaacha wahalifu wakirudi mtaani na kuendelea kutishia usalama wa watoto.

Pamoja na matukio ya kikatili kuendelea kuripotiwa mkoani mwanza tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa na serikali ya mkoa kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ambapo elimu imekuwa ikitolewa kwa njia ya radio na mikutano ya hadhara juu ya namna ya kutokomeza vitendo vya ukatili katika jamii.

Takwimu za hali ya matukio ya ukatili kwa watoto katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021 iliyotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum,jumla ya matukio yaliyoripotiwa na jeshi la polisi ni 11,499 huku mkoa wa Mwanza ukitajwa kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza ikiwa na matukio 500 ya ukatili kwa watoto.
Samson Marwa mganga wa wilaya ya Ilemela.
Said Kitinga katibu tawala wilaya.

No comments:

Powered by Blogger.