LIVE STREAM ADS

Header Ads

Jiji la Mwanza latakiwa kuweka taratibu rafiki za upangaji Soko Kuu, Stendi ya Nyegezi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com 
Halmashauri ya Jiji la Mwanza imetakiwa kuweka taratibu rafiki za upatikanaji wa vyumba vya biashara na vizimba kwenye miradi ya kimkakati ya Soko Kuu Mwanza na Stendi ya Mabasi Nyegezi ili kila mwananchi anayevutiwa kufanya biashara katika maeneo hayo apate nafasi bila vikwazo.

Rai hiyo imetolewa na diwani wa Kata ya Igoma, Mussa Ngolo wakati akichangia hoja kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kilichoketi Jumanne Mei 23, 2023 kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji ngazi ya Kamati kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2023/24.

Ngolo amesema kigezo cha kwanza kilichopendekezwa na Halmashauri hiyo ni lazima mfanyabiashara awe na leseni ili aweze kufanya biashara katika maeneo hayo hatua ambayo itawanyima fursa wananchi wengine ambao wanatamani kuitumia miradi hiyo kwa ajili ya kujipatia kipato.

"Miradi hii ya soko na stendi itakapoanza kufanya kazi itasaidia kuchochea uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla hivyo ni vyema Halmashauri ipitie upya taratibu za upatikanaji wa vyumba na vizimba ili wananchi waweze kunufaika na kuifurahia miradi hiyo" amesema Ngolo.

Kwa upande wake Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha amesema miradi ya mbalimbali ya kimkakati inalenga kuwanufaisha wananchi hivyo taratibu mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha lengo hilo linatimia.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Erick Mvati amesema ugawaji wa vyumba na vizimba katika miradi hiyo unafanywa kwa mujibu wa sheria na kanuni lakini kutokana na maombi ambayo yametolewa kwenye baraza hilo, watafanya marekebisho katika sheria hizo ili wananchi waweze kujitokeza kufanya biashara katika maeneo hayo.

Amesema mradi wa soko kuu utakapo kamilika utaweza kuchukua zaidi ya wafanyabiashara 1,400 na hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 87 huku mradi wa stendi ya Nyegezi ambayo tayari imekamilika ikitarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Erick Mvati akijibu hoja mbalimbali wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo.
Naibu Meya Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha akizungumza kwenye kikao hicho.
Diwani wa Kata ya Igoma, Mussa Ngolo akichangia hoja wakati wa kikao hicho.

No comments:

Powered by Blogger.