SMAUJATA waanzisha kampeni ya uchangiaji chakula mashuleni
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wananchi, Wazazi na Walezi wa Kata ya Manyoni mkoani Singida, wakiwa kwenye mkutano ulioandaliwa na Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Kata ya Manyoni kwa ajili ya kujadili utokomezaji wa ukatili katika kata hiyo na maeneo mengine na kuanzisha kampeni ya uchangiaji wa chakula mashuleni, uliofanyika jana Juni 2,2023 Shule ya Msingi Tambukareli na kuongozwa na Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata hiyo, Shujaa, Wallece Sechambo.
Na Dotto Mwaibale, Manyoni
Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Kata ya Manyoni mkoani Singida, wameanza kampeni ya kufa na kupona ya kuhamasisha jamii kuchangia upatikanaji wa chakula mashuleni ikiwa ni sehemu ya mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Juni 02, 2023 katika mkutano uliofanyika Shule ya Msingi ya Tambukareli wilayani humo na kuwahusisha wazazi na wananchi kwa ajili ya kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili na kuanzisha kampeni hiyo, Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata hiyo, Shujaa Wallase Shechambo alisema mikutano ya namna hiyo ya kuwahusisha wazazi na wananchi ni ya muhimu katika mustakabari mzima wa kupinga ukatili.
"Sisi kama SMAUJATA katika kata yetu tumeona ni vizuri kufanya mikutano ambayo tutawashirikisha wananchi, walezi na wazazi kwa lengo la kukaa pamoja ili kuzungumzia vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia na kutafuta mbinu za kutokomeza vitendo hivyo'" alisema Shechambo.
Alisema upo ukatili wa aina mbalimbali kama, ndoa za utotoni, ubakaji, ukatili wa kingono, kisaikolojia, kiuchumi, kipigo, kuwanyima watoto haki ya kwenda shule kusoma, ulawiti, ukeketaji, biashara haramu ya kusafirisha binadamu na mwingine mwingi unaofana na huo na kuwa kazi kubwa ya SMAUJATA ni kuupinga kwa nguvu aina zote za ukatili.
Shechambo alisema katika kata hiyo na wilaya nzima ya Manyoni kumekuwa na vitendo hivyo na kuwa wao kama SMAUJATA wamejipanga vilivyo kupambana na vitendo hivyo ambavyo si vizuri katika jamii na hata Mwenyezi Mungu havimpendezi.
Shechambo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi, wazazi na walezi mara watakaona au kubaini kuwepo kwa vitendo vyote vya ukatili kwenda ofisi ya kata hiyo au dawati la jinsia kituo kikuu cha Polisi wilayani humo kutoa taarifa ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa.
Mwenyekiti wa SMAUJATA wa Kata hiyo, Hossen Kheri alisema pamoja na kujadili suala la ukatili wa kijinsia pia waliona watumie mkutano huo kuanzisha kampeni ya kuhamasisha jamii kuchangia chakula ili wanafunzi waweze kupata chakula cha mchana wawapo shuleni kwani wamebaini baadhi ya watoto wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili kutokana na kudanganywa kwa kupewa pesa za kununulia chakula au kununuliwa na watu wenye nia mbaya na kujikuta wakinaswa katika mtego huo.
"Watoto wetu wanapokosa chakula shuleni ni rahisi kurubuniwa kwa kupewa hela kwa ajili ya kununulia chipsi na vyakula vingine hivyo shime wazazi tujitoe kusaidia kupata chakula ili kuwanusuru kwani tukiamua jambo ili linawezekana hakuna sababu ya kuisubiri Serikali kutufanyia suala hili," alisema Kheri.
Katibu wa SMAUJATA wa kata hiyo, Sara Yohana naye aliunga mkono suala hilo la kuhamasisha wazazi kupata chakula cha watoto wakiwa shuleni na kueleza kukosekana kwa chakula hicho kuna madhara makubwa kwa wanafunzi ikiwa pamoja na kutozingatia vizuri masomo.
"Suala hili wala sio la kuiachia Serikali ni letu sote na njaa haina mtu mkubwa wala mtoto na mdogo kwani ukipita muda wa kula hata mtu mzima utakuta anakuwa kimya kwa maumivu ya njaa sembuse mtoto," alisisitiza Yohana.
Katika tukio lingine kikosi kizima cha SMAUJATA katika kata hiyo kimeweza kuibua tukio la watoto watatu wa familia moja ambao walikuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili na kushindwa kupelekwa shuleni licha ya mtoto wa kwanza kuwa na umri wa miaka 13, wa pili miaka tisa na mdogo wao akiwa na miaka saba.
Watoto hao inadaiwa tangu wazaliwe hawajawahi kupelekwa shuleni zaidi ya kuwepo nyumbani wakifanyiwa vitendo vya ukatili lakini jana baada ya viongozi hao wa SMAUJATA kupata taarifa hiyo walikwenda kutoa elimu kwa wazazi wa watoto hao kuhusu umuhimu wa watoto hao kupata elimu ambao walikiri kufanya makosa ambapo viongozi hao walikwenda kuzungumza na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Tambukareli ambaye alikubali kuwapokea na mwezi ujao shule zitakapofunguliwa wataanza kusoma kwa utaratibu atakao wapangia.
Kikosi kazi cha Mashujaa wa SMAUJATA kilichofanya kazi hiyo kubwa kikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wao Shujaa Wallece Shechambo ni Hossen Kheri, Sarah Yohana, Joyce Peter, Henry Mallya, Neema Massabuni, Zena Salum na Mary Saileni.
Viongozi wa SMAUTA wa Kata ya Manyoni wakitoa elimu kwa moja ya familia ambayo watoto wao watatu walikuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia na kujimwa haki yao ya msingi ya kupelekwa shuleni kupata elimu.
No comments: