LIVE STREAM ADS

Header Ads

KAMPUNI YA RADDY ENERGY YA TANZANIA KUNUNUA MITAMBO YA UZALISHAJI UMEME KUTOKA KAMPUNI YA SIEMENS YA USWIDI KWA DOLA MILIONI 320

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Balozi wa Tanzania nchini Uswidi, Mhe. Mobhare Matinyi (wa nne kutoka kushoto mstari wa mbele), akiwa pamoja na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Raddy Energy ya Tanzania, Ramadhani Mlanzi (kulia kwake), katika picha ya pamoja na wawakilishi wa taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi, kampuni ya Siemens Energy, Benki ya CRDB, Ubalozi na Raddy Energy, jijini Stockholm, mara baada ya kikao kilichofanyika siku chache zilizopita kukamilisha mchakato wa ununuzi wa mitambo minne ya kuzalisha umeme wa gesi itakayoletwa nchini ili kuimarisha uzalishaji wa umeme nchini.


 Kikao cha pamoja baina ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uswidi, kampuni ya Raddy Energy, Benki ya CRDB na wawakilishi wa taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi wakiendelea na kikao jijini Stockholm, hivi karibuni.

***

Kampuni ya Raddy Energy Solution Limited ya Tanzania imeingia makubaliano ya kununua mitambo minne ya kuzalisha umeme kwa njia ya gesi asilia wa jumla ya megawati 177 kutoka kampuni ya Siemens Energy ya Uswidi (Sweden) kwa thamani ya dola za Marekani milioni 320.

Ununuzi wa mitambo hiyo itakayowasili nchini Tanzania na kufungwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2027, umewezeshwa na Benki ya CRDB kama mshirika wa ndani. Kampuni ya Raddy Energy ni kampuni dada na kiwanda cha Raddy Fibers kilichopo Mkuranga, mkoani Pwani.

Katika kufanikisha mradi huu, Benki ya CRDB itafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi ikiwemo Wakala wa Mikopo ya Mauzo ya Nje wa Uswidi (EKN), Shirika la Mikopo ya Mauzo ya Nje la Uswidi (SEK), Taasisi ya Fedha za Maendeleo ya Uswidi (Swedfund), Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uswidi (SIDA) na Taasisi ya Mauzo ya Nje na Uwekezaji ya Uswidi (Business Sweden), ambazo zote ni taasisi za serikali.

Baraza la Kimataifa la Viwanda la Uswidi (NIR) nalo litakuwa sehemu ya ushauri wa timu ya kimataifa itakayofanikisha mradi huu, ambao ni mwanzo tu kwani kampuni ya Raddy Energy inapanga kufikisha uzalishaji wa megawati 1,000 ifikapo mwaka 2030 ili kuiwezesha Tanzania kuwa na umeme wa uhakika kwa matumizi ya ndani na kuuza nje ya nchi.

Mnamo tarehe 10 hadi 13 Desemba, 2025, watendaji wa kampuni ya Raddy Energy walifanya ziara ya kimkakati nchini Uswidi chini ya uratibu wa Ubalozi wa Tanzania na kukutana na watendaji wa Siemens Energy na taasisi za fedha za Serikali ya Uswidi kwenye ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje, jijini Stockholm, na baadaye kuzuru makao makuu ya Siemens, mjini Finspäng.

Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Balozi wa Tanzania, Mhe. Mobhare Matinyi na Raddy Energy ilikuwa na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mwendeshaji, Bw. Ramadhan Hassan Mlanzi na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara na Miradi, Bw. Ediphine Masase. Timu ya Benki ya CRDB inayohusika na uchakataji wa miradi mikubwa iliongozwa na Bw. Musa Lwila, Bw. Saidi Salehe na Bw. Andrew Mbunda.

Kadhalika, timu ya Siemens Energy iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Ufadhili wa Miradi, Bw. Joakim Tornberg na Meneja Mwandamizi wa Mauzo, Bi. Christiane Carlsson katika kikao hicho ambapo timu ya Serikali ya Uswidi iliongozwa na Mshauri Mwandamizi wa Biashara na Uendelezaji kwa bara la Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bi. Pia Roed. 

Wawakilishi wa taasisi zingine za Serikali ya Uswidi walikuwa kama ifuatavyo: Bi. Anna Liberg (Business Sweden); Bw. Maximilian Jönsson (SIDA); Bw. Johan Heiskala (Swedfund), Bw. Klas Lindgren (EKN) na Bw. Pontus Davidsson (SEK), na Bi. Christine Bäckström (NIR).

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Balozi Matinyi alitumia fursa hiyo kuelezea mwelekeo wa ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden katika kuimarisha biashara na uwekezaji na kusisitiza kwamba Tanzania ina fursa zaidi katika sekta za madini, viwanda, kilimo cha biashara, usafirishaji, utalii pamoja na teknolojia na ubunifu.

Imetolewa na:

Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uswidi

Stockholm, 19 Desemba, 2025.

No comments:

Powered by Blogger.