ZOEZI LA USAFI LAFICHUA ATHARI ZA UTUPAJI HOLELA WA TAKA BAHARINI
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
UCHAFUZI wa mazingira ya bahari, unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na utupaji holela wa taka ngumu hususan chupa za plastiki katika mito na mitaro, umetajwa kuwa tishio kwa afya za binadamu, uhai wa viumbe wa baharini pamoja na sekta ya utalii jijini Dar es Salaam.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw. Edward Mpogolo, wakati wa zoezi la usafi katika Fukwe ya Dengu iliyopo Bahari ya Hindi, lililolenga kuhamasisha usafi wa mazingira na kulinda fukwe za Jiji la Dar es Salaam.
Bw. Mpogolo amesema taka zinazotupwa ovyo katika maeneo ya makazi na mitaro huishia baharini kupitia mkondo wa maji, hali inayosababisha uchafuzi mkubwa wa fukwe na kuathiri moja kwa moja afya za wananchi pamoja na mazingira ya bahari.
Amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vya uchafuzi wa mazingira, na kutoa onyo kali kwa wananchi wanaoendelea kujihusisha na tabia ya utupaji holela wa taka, akibainisha kuwa sheria na kanuni za mazingira zitatekelezwa kikamilifu dhidi ya watakaobainika kukiuka.
Zoezi hilo la usafi limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la LASDGs na JUZA, mashirika yanayojishughulisha na uhifadhi wa mazingira na usimamizi wa taka ngumu jijini Dar es Salaam. Kupitia zoezi hilo, wananchi wamehamasishwa kubadilisha mtazamo wao na kuwa sehemu ya suluhisho la kulinda mazingira yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JUZA, Bw. Nassib Kitabu, amesema juhudi za pamoja kati ya Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi ndizo nguzo kuu ya kuhakikisha mazingira ya bahari na fukwe yanabaki salama na safi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Bw. Mpogolo ameongeza kuwa Serikali ina mkakati wa kuboresha usafi katika fukwe zote za Jiji la Dar es Salaam ili kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Wadau wa mazingira, akiwemo Dkt. Erick Mwate na Bi. Mariam Lulida, wamepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali pamoja na mashirika ya kiraia katika kulinda fukwe, wakisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kufanikisha juhudi hizo.
Wamesema kulinda mazingira ya bahari si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha fukwe na vyanzo vya maji vinabaki salama, safi na endelevu kwa manufaa ya Taifa.





No comments: