LIVE STREAM ADS

Header Ads

USHIRIKIANO WA SERIKALI NA WORLD VISION WAIMARISHA AFUA ZA LISHE SHINYANGA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali kwa kushirikiana na shirika la World Vision Tanzania limeendelea kuimarisha afua za lishe na afya ya uzazi katika Mkoa wa Shinyanga kupitia utekelezaji wa mradi wa Grow ENRICH unaotekelezwa katika Halmashauri ya Shinyanga Mjini na Kishapu.

Hayo yamebainishwa leo Januari 26, 2026 Jijini Mwanza katika jukwaa la wadau wa maendeleo, katika Kujifunza na majadilino kupitia mradi wa Grow ENRICH, wa miaka mitano unaotekelezwa katika Halmashauri mbili za Mkoa wa Shinyanga namna ambavyo umesaidia kupunguza utapiamlo na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu lishe bora.

Mtaalam wa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Grace Mushi, amesema mradi wa Grow ENRICH unaofadhiliwa na world vision Tanzania unatekeleza shughuli mbalimbali za afya pamoja na lishe na serikali ya jamahuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza mpango kazi jumuhishi maswala ya lishe Kwa mwaka 2021-2022 hadi 2025-2026.

Mushi ameeleza kuwa Tanzania inakabiliwa na matatizo makuu matatu ya lishe ikiwa ni pamoja na utapiamlo, lishe pungufu, na lishe ya kuzidi ambapo ameeleza kuwa Kwa watoto, udumavu uko asilimia 30, uzito pungufu asilimia 12, na utapiamlo ukondefu asilimia 3.

Kwa upande mwingine amefafanua kuwa Upungufu wa madini na vitamini unawapata watoto na wanawake, ambapo asilimia 59 ya watoto na asilimia 42 ya wanawake wa umri wa kuzaa wana upungufu wa damu, na Utapilomlo wa lishe ya kuzidi unashika kasi, ambapo asilimia 36 ya wanawake na asilimia 4 ya watoto wana uzito uliozidi.

"Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanya mambo mengi, ikiwemo kutoa matone ya vitamini A kwa watoto, kutoa elimu kwa wananchi kupitia vituo vya afya na jamii, na kufanya urutubishaji wa chakula kwa kuongeza madini na vitamini kwenye vyakula" alisema Mushi.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Afisa Lishe wa Mkoa wa Shinyanga, Mussa Makungu, amesema kuwa mradi wa Grow ENRICH unatekelezwa katika kata 6 na vijiji 29 katika Halmashauri ya Shinyanga DC, huku Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ukitekelezwa katika kata 3 na vijiji 12.

Makungu amesema kuwa mradi umechangia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na kuondoa mila potofu zilizokuwa zinaathiri hali ya lishe kwa watoto, hasa katika maeneo ya vijijini.

"Kumekuwa na mabadiliko chanya katika ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya lishe ngazi ya familia, hali iliyokuwa changamoto kubwa awali, kupitia World Vision, vikundi vya kijamii viliundwa kwa lengo la kutoa elimu ya lishe, kuwahamasisha mama wajawazito kuwahi kliniki pamoja na kutambua dalili hatarishi kabla ya changamoto kutokea.

Kwa upande wake, Mratibu wa Sekta ya Afya na Lishe kutoka Shirika la World Vision Tanzania, Dkt. Stanford Kaserwa alisema mradi umefikia takribani watu laki 123 elfu sawa na asilimia 91 ya walengwa, shule 55 zimefikiwa katika masuala ya vyakula vilivyoimarishwa kwa virutubishi, pamoja na kaya zaidi ya 400.

Naye Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Kivulini, Yasin Ally, alisema kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Takwimu ya Taifa, kiwango cha utapiamlo katika Mkoa wa Shinyanga kilikuwa asilimia 30, lakini kupitia mchango wa World Vision, Kivulini na wadau wengine, kiwango hicho kimeshuka hadi asilimia 27.
Afisa lishe mwandamizi kutoka Wizara ya Afya, Grace Mushi, akielezea namna mradi wa Grow ENRICH unavyofanya kazi Kwa kushirikiana serikali.
Mratibu wa Sekta ya afya na lishe Shirika la World Vision Tanzania, Dkt. Stanford Kaserwa akielezea jinsi gani shirika la World Vision lilivyosaidia kupunguza swala utapiamlo kupitia mradi wa GROW ENRICH Mkoani Shinyanga.
Kaimu Afisa Lishe wa Mkoa wa Shinyanga, Mussa Makungu, akielezea mradi wa GROW ENRICH uliweza kupunguza utapiamlo katika Mkoa wa Shinyanga na kuondoa Mila potofu katika maswala yap lishe.

No comments:

Powered by Blogger.