LIVE STREAM ADS

Header Ads

VIONGOZI MWANZA WAONGOZA ZOEZI LA UPANDAJI MITI KUADHIMISHA SIKU YA KUZALIWA RAIS SAMIA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi wameongoza zoezi la kupanda miti zaidi ya 1,000 katika Shule ya Sekondari Kakebe iliyoko Kata ya Igoma jijini Mwanza.

Zoezi hilo limefanyika Jumanne Januari 27, 2026 ikiwa ni sehemu ya kushiriki kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza baada ya kupanda miti hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda aliwataka wanafunzi na uongozi wa shule hiyo kuitunza vizuri miti iliyopandwa ili iweze kukua na kuyafanya mazingira kuwa ya kijani

"Tumepanda miti zaidi ya 1,000 ikiwemo ya matunda, kimvuli na urembo. Ili iweze kustawi vizuri inahitaji matunzo hivyo jitahidini sana kuitunza ili ilete tija kwenu na jamii kwa ujumla" alisema Mtanda.

Aidha Mtanda aliiomba jamii kuwa na utaratibu wa kupanda miti kwenye Kaya zao ili waweze kupata matunda yatakayowasaidia kuboresa afya zao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi alisema miti inasaidia kuondoa hewa ukaa na kuwa na mazingira mazuri ya kufundishia hivyo amewasisiatiza wanafunzi kuitunza vizuri.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kakebe, Masome Masome alisema atashirikiana na uongozi wa shule hiyo kuhakikisha miti hiyo inakua.

Mwl. Isaac Otieno ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Kakebe alisema kwa mwaka 2026 shule hiyo imepata wanafunzi 305 wa kidato cha kwanza, wavulana 123 na wasichana 182.

Pia alitoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuifanya shule hiyo kuwa ya kijani.

"Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu na tunampongeza kwa kuongeza umri, tunamuombea kwa Mungu awe na afya njema ili azidi kutuletea maendeleo katika shule yetu, mkoa wetu na taifa kwa ujumla" alisema Mwl. Otieno.

Nao baadhi ya wanafunzi walieleza furaha yao baada ya kuletewa miti ambapo walisema watajitahidi kuimwagilizia na kuiwekea mbolea ili iweze kukua vizuri ikiwa ni ishara pia ya kumbukumbu ya kuzaliwa Dkt. Samia ambaye amekuwa akisisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akishiriki zoezi la upandaji miti.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akishiriki zoezi la upandaji miti.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akimwagilia mche maji.
Mwanafunzi Shule ya Sekondari Kakebe akipanda mche.

No comments:

Powered by Blogger.