LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mapokezi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ofisini

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (kushoto) akisalimiana na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (kulia), baada ya kuwasili katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dodoma Septemba 04, 2023. Wa pili kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, (pili kulia) na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali wa Wizara ya Nishati, Ziana Mlawa( kulia).
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akisaini kitabu cha wageni baaada ya kuwasili katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma.
Watumishi wa Wizara ya Nishati wakiwa katika tukio la kumpokea Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga katika Ofisi za Wizara, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (kulia) akimkaribisha Naibu Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma.
Naibu Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili ofisini.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizungumza na watumishi wa Wizara ya Nishati baada ya kumpokea Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizungumza na watumishi wa Wizara ya Nishati.
***

Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga wamepokelewa rasmi na Menejimenti na Watumishi wa Wizara ya Nishati katika Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo jijini Dodoma baada ya kuapishwa na Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kushika nyadhifa hizo.

Akizungumza na Menejimenti na Watumishi hao tarehe 04 Septemba 2023, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amemshukuru Rais, Dkt. Samia kwa kumuamini katika kuisimamia Sekta ya Nishati na ameahidi kuwa yeye pamoja na Naibu Waziri watafanya kazi kwa bidii na ufanisi ili kuitendea haki imani hiyo.

Dkt. Biteko ameeleza kuwa, kazi iliyo mbele ni kuhakikisha kuwa huduma ya nishati inawafikia wananchi wote na kwamba, pamoja kazi nzuri iliyofanyika ya kuimarisha Sekta ya Nishati, bado kuna nafasi ya kufanya kazi hiyo vizuri zaidi ili nishati ya uhakika ipatikane, na hiyo ndiyo azma na matarajio ya Rais na wananchi kwa ujumla.

“Kama watu hawapati umeme, kama watu hawapati nishati wanayoihitaji, hata tukivaa suti za namna gani tunakuwa hatuna maana na tutakuwa na tunasemwa kila siku, kiu yangu ni kuona tunafanya kazi kwa viwango ili huduma ya nishati iwafikie wananchi wote” amesisitiza Dkt. Biteko.

Amempongeza aliyekuwa Waziri wa Nishati, January Makamba kwa juhudi alizofanya kuendeleza Sekta na kuahidi kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati itaendelea ili kufanya nchi kuwa na nishati ya uhakika.

Dkt. Biteko ameshukuru kwa mapokezi mazuri aliyopata wakati akiwasili Wizara ya Nishati na ameeleza kuwa atafanya kazi kwa pamoja na watumishi wa Wizara ili kuiendeleza Sekta na amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa amani.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amemshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa imani aliyompatia ili kuweza kuhudumia Sekta ya Nishati kama Mbunge aliyetoka katika kundi la vijana na ameahidi uchapakazi, weledi na ufanisi katika kazi zake.

Kapinga ameeleza kufarijika kwake kwa kurudi katika Sekta ya Nishati kwani tayari alishaanza kuwa na uzoefu nayo wakati akihudumu kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Amemshukuru Mhe. Rais pia kwa kumwezesha kufanya kazi chini ya Dkt. Doto Biteko kwani ana uzoefu katika uongozi na Sekta ya Nishati hivyo chini ya uongozi wake ataendelea kukua na kufanya kazi kwa ufanisi.

Ameahidi kutoa ushirikiano kwa Watumishi wa Wizara ya Nishati na pia amewaasa Watumishi hao kumpa ushirikiano ili kwa pamoja waweze kutekeleza majukumu yatakayoendeleza Sekta ya Nishati na kusisitiza kuwa heshima ya mtu ni kazi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amempongeza Dkt.Doto Biteko kwa kuteuliwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati pia amempongeza Judith Kapinga kwa kuaminiwa na Rais kuwa Naibu Waziri wa Nishati.

Mhandisi Mramba, amewakaribisha viongozi hao katika Wizara ya Nishati, na kueleza kuwa Wafanyakazi watatoa ushirikiano kwa viongozi hao ili kuweza kutekeleza majukumu yao kazi kwa ufanisi mkubwa.

No comments:

Powered by Blogger.