LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali yatoa vifaa tiba Kituo cha afya Msange

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Afisa Mauzo wa MSD Kanda ya Dodoma, Omari Mosi akizungumza kwa niaba Meneja wa MSD wa kanda hiyo, Mwanashehe Jumaa wakati akikabidhi jenereta la dharura litakalotumika katika Kituo cha Afya Msange kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida Februari 7, 2024.
.................................................


Na Dotto Mwaibale, Singida
Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imekikumbuka Kituo cha Afya cha Msange kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwa kutoa fedha jumla ya Sh.Milioni 150 kwa ajili ya kununua vifaa tiba.

Afisa Mauzo wa MSD Kanda ya Dodoma, Omari Mosi akizungumza kwa niaba Meneja wa MSD wa kanda hiyo, Mwanashehe Jumaa wakati wa kukabidhi jenereta la dharura litakalotumika katika kituo hicho lenye thamani ya Sh.Milioni 65.7 alisema kati ya fedha hizo zilizotolewa tayari wamekwisha peleka vifaa vyenye thamani ya Sh.Milioni 98.3.

"Vifaa vingine vilivyobaki vitaendelea kupelekwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu MSD itahakikisha vinafika na vinatumika kutoa huduma za matibabu kwa wananchi" alisema Mosi.

Alisema katika zoezi la kupeleka vifaa tiba hivyo kwenye vituo vya afya Ofisi ya Rais TAMISEMI imetenga jumla ya Sh.Milioni 700 kwa ajili ya manunuzi ya vifaa hivyo na kuwa Kituo cha Afya Msange kimenufaika na fedha hizo.

Alisema katika Halmashauri hiyo vituo sita vimetengewa fedha kwa ajili ya vifaa hivyo ambavyo vinaendelea kupokelewa.

Mosi alisema jukumu kubwa la MSD ni kununua, kutunza, kuzalisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara katika vituo vyote vya Serikali vilivyopo nchini na kueleza kuwa MSD wamedhamiria kuokoa maisha ya watu.

Diwani wa Kata ya Msange ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Eliya Digha akizungumza wakati akipokea vifaa hivyo alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali watanzania hususani wananchi wa halmashauri hiyo na Kata ya Msange.

Alisema kituo hicho kimejengwa kwa fedha za Serikali jumla ya Sh.Milioni 500 na kuwa wametumia Sh.Milioni 200 kwa ajili ya manunuzi ya vifaa tiba.

Digha aliishukuru Serikali na MSD kwa kuwapelekea jenereta hilo la dharura ambalo linakwenda kusaidia wakati umeme utakapokuwa unakatika.

Wakazi wa Kata hiyo Hamisi Ramadhani na Greta Nyonyi waliishukuru Serikali na MSD kwa kuwapelekea jenereta hilo ambalo litakuwa mkombozi kwao.

"Tulikuwa na changamoto kubwa baada ya umeme wa kawaida kukatika hasa kwa upande wa wajawazito ambao walikuwa wakitakiwa kufanyiwa upasuaji lakini kwa jenereta ili tuliloletewa na MSD tuna kila sababu ya kutoa shukurani zetu kwa viongozi wetu" alisema Nyonyi.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Noel Mchau alisema jenereta hilo litawafanya kuwa na umeme wa uhakika na kuweza kutoa huduma za matibabu kwa urahisi na haraka kwa masaa 24.Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Noel Mchau akizungumza wakati wa mapokezi hayo.
Diwani wa Kata ya Msange ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Eliya Digha akizungumza wakati akipokea vifaa hivyo.
Mkazi wa Kata hiyo Greta Nyonyi akiishukuru Serikali na MSD kwa niaba ya wanawake wa Kata hiyo kwa kuwapelekea jenereta katika kituo hicho cha afya.
Mapokezi ya jenereta hilo yakifanyika. Kutoka kushoto ni Afisa Mauzo wa MSD Kanda ya Dodoma, Omari Mosi, Mfamasia wa kituo hicho cha afya, Isengwa Mathias na Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Noel Mchau.
Afisa Mauzo wa MSD Kanda ya Dodoma, Omari Mosi, akimkabidhi jenereta hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Eliya Digha (kulia) Katikati ni Mwakilishi wa Mbunge wa Jimbo hilo, Amina Senge.
Wananchi wa Kata ya Msange na viongozi wao wakionesha furaha yao wakati wakipokea jenereta hilo.
Gari la MSD likishusha jenereta hilo.

No comments:

Powered by Blogger.