LIVE STREAM ADS

Header Ads

TBS yawataka wafanyabiashara na wazalishaji wa vyakula kuzingatia usalama

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa za Vyakula nchini kuzingatia usalama wa bidhaa hizo kabla ya kumfikia mlaji kwa lengo la kulinda afya kwa mlaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Februari 13,2024 Kaimu Meneja wa Kitengo cha kufanya Tathimini ya vihatarishi vya chakula (TBS) Dkt. Ashura Katunzi amesema usalama wa chakula ni wajibu wa kila mtu katika mnyororo wa thamani,kuanzia kwa mzalishaji hadi kinapomfikia mlaji.

Amesema kuwa chakula kisipokua katika hali ya salama kinaweza kusababisha madhara ya kiafya na hata kusababisha vifo na kuzorotesha uchumi pamoja na maendeleo ya watu.

Dkt. Katunzi amebainisha mbinu zitakazosaidia kuwa na chakula salama ambapo amesema katika maandalizi ya chakula migahawani na Viwandani waandaji wanapaswa kuweka mazingira safi na kunawa mikono kwa sabuni kabla na baada ya maandalizi hayo.

Amesema kuna umuhimu mkubwa wa kutenganisha chakula kibichi na kilicho tayari kuliwa, kwa sababu kile kilichopikwa kitakuwa kimezingatia kanuni za usafi "huwezi kuchanganya nyama iliyopikwa na nyama mbichi katika friji Dkt. Katunzi ameeleza.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa chakula kinatakiwa kuhifadhiwa katika joto salama ili kuhakikisha hakizalishi vimelea vya wadudu na kutumia malighafi ambazo ni bora kwa lengo la kulinda afya ya mlaji.

"Wenzetu wale wanaofuga wanyama wasiende kuuza wanyama wakiwa na siku chache wametumia madawa, wataalamu wanaeleza mnyama aliepewa dawa akae muda gani nyama yake iweze kuliwa. Na wale wanaolima matunda na mboga yakipelekwa sokoni, mlaji anaweza asijue mboga hii imepuliziwa dawa kwa muda gani". amesema Dkt. Katunzi.

Kwa Upande wake Kaimu Meneja wa Ukaguzi na Uzingatiaji wa Sheria (TBS), Moses Mbambe amesema kuwa sheria inawataka wazalishaji wa chakula kuzingatia viwango na waagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi kusajili maeneo ambayo usindikaji wa bidhaa husika unafanyika ili kuhakikisha ubora na usalama.

Aidha Meneja Ukaguzi huyo ametoa onyo kwa wafanyabiashara wa bidhaa hizo wanaofanya ulaghai kwa kuuza bidhaa ambazo muda wake wa matumizi umepita, kuachana na tabia hiyo kwa kuuza bidhaa ambazo hazijazingatia mahitaji ya viwango.
Kaimu Meneja wa Kitengo cha kufanya tathimini ya vihatarishi vya chakula (TBS) Dkt. Ashura Katunzi akizungumza na waandishi wa habari Februari 13, 2024 katika Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Meneja wa Ukaguzi na Uzingatiaji wa Sheria (TBS), Moses Mbambe akizungumza na waandishi wa habari Februari 13, 2024 katika Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Jijini Dar es Salaam

No comments:

Powered by Blogger.