LIVE STREAM ADS

Header Ads

Benki ya CRDB yanogesha michuano ya kombe la shirikisho

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Michuano ya soka ya kombe la shirikisho ambayo sasa inajulikana kama CRDB Bank Federation Cup, imeendelea kupamba moto katika hatua ya 16 bora huku benk ya CRDB inayodhamini michuano hiyo ikijipanga vyema kutoa zawadi mbalimbali kwa wachezaji ili kuongeza hamasa zaidi ya ushindani.

Katika mchezo uliopigwa Aprili 04, 2024 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, wenyeji wa mchezo huo timu ya Singida Fountain Gate walikubali kichapo cha goli tatu kwa nunge kutoka Tabora United.

Katika mchezo huo, mchezaji wa Tabora United, Najimu Mussa aliibuka mchezaji bora na kujinyakulia kitita cha shilingi laki tano kutoka kwa mdhamini, benki ya CRDB.

"Benki ya CRDB imekuwa mdhamini mkubwa wa kombe la shirikisho, na leo niko hapa kumkabidhi mchezaji bora wa mchezohuu, Najimu Mussa kutoka Tabora United. Tutamfungulia akaunti ya CRDB hapa hapa na kumwekea fedha zake" alisema Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta.

Sitta alisema benki ya CRDB ikiwa kama mdhamini mkuu wa michuano hiyo ya kombe la shirikisho (CRDB Bank Federation Cup) itaendelea kutoa motisha na zawadi mbalimbali kwa wachezaji ili kunogesha zaidi michuano hiyo.

Naye mchezaji wa Tabora United, Najimu Mussa alisema hatua hiyo ya mdhamini, benki ya CRDB kutoa zawadi kwa wachezaji inatoa hamasa kwa timu shiriki kucheza vizuri uwanjani.

Itakumbukwa Aprili 02, 2024 benki ya CRDB iliingia makubaliano na shirikisho la soka Tanzania (TFF) kudhamini michuano ya kombe la shirikisho kwa udhamini wa shilingi bilioni 3.79 kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia msimu huu wa mwaka 2023/24 ambao umefikia hatua ya 16 bora.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta (kushoto) akimkabidhi hundi ya shilingi laki tano mchezaji wa Tabora United, Najimu Mussa (katikati) baada ya kuibuka mchezaji bora kwenye mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate. Kulia ni Katibu wa Chama cha Soka Mkoa Mwanza.
Mchezaji wa Tabora United, Najimu Mussa akisajiliwa akaunti ya benki ya CRDB kwa ajili ya kuwekewa fedha alizozawadia.
Tazama BMG TV hapa chini
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA

No comments:

Powered by Blogger.