LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Mkuu ashiriki kongamano la JUMIKITA jijini Dar

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA) imeandaa kongamano la miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake na kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kujadili masuala yatakayoimarisha zaidi jumuiya hiyo.

Kongamano hilo limefanyika Chuo Kikuu cha Dar es salaam Jumanne Mei 21, 2024 likiambatana pia na mjadala kuhusu miaka mitatu ya Rais Dkt. Suluhu Hassan pamoja na maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani 2024.
Akifungua kongamano hilo, mgeni rasmi Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema mitandao ya kijamii imerahisisha upatikanaji wa taarifa na hivyo kutoa rai kwa wanahabari kufanya kazi kwa weledi kwa maslahi ya jamii.

Amesema Serikali imechukua hatua ya kufanya maboresho ya Sheria na Kanuni mbalimbali za Habari ili kutoa fursa kwa waandishi wa habari kufanya kazi kwa uhuru na kuifurahia kazi yao.

"Niwapongeze JUMIKITA kupitia kongamano hili, hii ni moja ya njia ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kuelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii" amesema Majaliwa.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia, sekta ya habari imepiga hatua na watanzania wanapata taarifa mbalimbali za maendeleo kupitia vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii.
Majaliwa amesema pia Dkt. Samia ameendelea kuimarisha ulinzi na usalama ndani na nje ya nchi, kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi mbalimbali duniani, kuendeleza na kusimamia tuzu za taifa ambazo ni umoja, mshikamano, utulibu na amani na kuifanya Tanzania kuwa kimbilio kwa nchi zilizopoteza matumaini.

"Ni muhimu tukaendelea kumuunga mkono Rais wetu katika jitihada anazozifanya kuimarisha sekta mbalimbali za uzalishaji kama kilimo, mifugo, uvuvi, madini, nishati, afya, maji, elimu, TEHAMA, uwekezaji na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati" amesema Majaliwa.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema sekta ya habari nchini imepiga hatua katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

"Hatujafika tunakokusudia lakini tulipo leo si tulipokuwa jana. Tunataka wanahabari waanze kujisimamia wenywe. Akikosea apambane na baraza la wanahabari na siyo Serikali kuingilia;

Hata sasa suala la kukamatana halipo tena ndo maana tumepanda kwenye uhuru wa habari kutoka nafasi ya 143 hadi 97" amesema Nnauye akimpongeza Rais Dkt. Samia kwa mchango wake wa kukuza sekta ya habari. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila amekiri kuwa Tanzania imepiga hatua katika eneo la utawala bora, demokrasia na uhuru wa habari hasa katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan huku ukuaji wa teknolojia ya habari ukirahisisha upashaji habari.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasili ukumbi wa Chuo Kikuu Dar es salaam kushiriki kongamano la JUMIKITA.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa ukumbini kwenye kongamano la JUMIKITA. Kushoto ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.
Mwenyekiti wa JUMIKITA Taifa, Shaaban Matwebe amesema kongamano hilo linatoa fursa kwa wanahabari wa mtandaoni kuketi pamoja na kujadiliana namna bora ya kuimarisha utendaji kazi wao.

"Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kipindi chake cha miaka mitatu, mabadiliko yaliyofanyika yametoa fursa kwa vijana kujiajiri mitandaoni" amesema Matwebe.

Mada mbalimbali zimewasilishwa kwenye kongamano hilo ambapo Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP. David Misime ametoa rai kwa waandishi wa habari wa mitandao ya kijamii kutumia vyema majukwaa yao kutoa habari sahihi, zenye mizania sawa na sizizopotofu kwa ajili ya manufaa ya taifa.

Naye Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji TCRA, John Daffa amesema mitandao ya kijamii imetoa fursa kwa waandishi wa habari. Amesema hadi kufikia Machi 2024 kulikuwa na watumiaji wa Intaneti milioni 36 huku wenye simu janja wakiwa ni milioni 20 ambapo hiyo ni fursa kwa wanahabari kufikisha matangazo na maudhui na kijipatia kipato.
Mtangazaji na mwanamaudhui wa mtandaoni, Millard Ayo ameomba Serikali kupita Wizara ya Habari na TCRA kuangazia upya gharama kubwa za ada ya leseni ambayo imeshuka kutoka milioni moja hadi laki tano kwa mwaka ili kuwapa fursa vijana wanaoanzisha vyombo vya habari mtandaoni. 

Pia ameomba Serikali kuwa mlezi badala ya kutoza faini hadi milioni tano pale wanapoonekana kukinzana na sheria katoka utoaji maudhui mtandaoni. 

Mwana maudhui mtandaoni, Godlitsen Malisa ametoa rai kwa Serikali kuwasaidia vijana wanaojiajiri kupitia mitandao ya kujamii ili wafanye shughuli zao kwa weledi badala ya kuandaa Sheria kali za kuwashughulikia.

Mkurugenzi wa TMF, Dastan Kamanzi amesema taasisi hiyo iko tayari kuwajengea uwezo kimafunzo na kiuchumi waandishi wa habari wa mitandao ya kijamii ili kuwawezesha kuepuka uandishi wa habari wa kijamii (Citizen Journalism) na kufanya uandishi wa kuhoji/ kiuchunguzi (Investivative Journalism) kwa maslahi mapana ya jamii.
Wanahabari wa mitandao na wadau mbalimbali wakiwa kwenye kongamano la JUMIKITA jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa JUMIKITA Taifa, Shaaban Matwebe akiwa kwenye kongamano hilo.
Mwakilishi wa TCRA akizungumza kwenye kongamano hilo.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime akitoa mada ya usalama kwenye kongamano hilo.
Mkuu wa Mkoa Dar es salaam, Albert Chalamila (kushoto) akiwasili kwenye kongamano hilo.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (katikati), Msemaji wa Serikali, Mbare Matinyi (wa pili kushoto) na wanahabari wa mitandao ya kijamii wakiteta jamba kando ya kongamano hilo.
Wanahabari wa mitandao ya kijamii.
Washiriki wakiwa kwenye kongamano la JUMIKITA jijini Dar es salaam.
Mwanamaudhui wa mtandaoni, Godlitsen Malisa akizungumza kwenye kongamano hilo.
Waandishi wa Habari wa Mitandaoni wakiwa kwenye kongamano hilo ambalo limejumuisha washiriki kutoka Kanda ya Ziwa, Kaskazi, Kusini, Nyanda za Juu na Pwani.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG

No comments:

Powered by Blogger.