LIVE STREAM ADS

Header Ads

BITEKO: Fursa kwa mtoto wa kike ianzie ngazi ya familia

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameitaka jamii kuongeza nguvu ya kumpa fursa ya elimu mtoto wa kike kuanzia ngazi ya familia ikiwa ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii.

Dkt. Biteko alisema hayo jijini Dar es Salaam katika Kongamano la “citizen rising woman” ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani machi o8, 2025.

“Tuanze nalo katika ngazi ya familia kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo katika jamii. Maendeleo ya jamii yeyote ile huanzia katika ngazi ya familia. Hivyo, sisi tumwendeleze mwanamke kwa kumpatia na kumfungulia fursa mbalimbali za elimu” alisema Dkt. Biteko.

Alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika maeneo kadhaa ikiwemo kuwawezesha wanawake kujikomboa dhidi ya umaskini, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, kushiriki katika nafasi mbalimbali za maamuzi na hivyo kupiga hatua katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Wakati tunaposherehekea siku ya wanawake duniani, ni muhimu pia kusherehekea mafanikio tuliyopata katika kutatua changamoto za haki za wanawake hasa katika vipengele 12 vya Mwongozo wa mkutano wa Beijing” alisema Dkt. Biteko.

Aidha alisema wakati Dunia inaasherehekea siku ya wanaweke kimataifa, kuna ulazima wa kutambua na kuzifanyia kazi changamoto zilizopo huku akizitaja baadhi yake kuwa ni ukatili wa kijinsia hasa maeneo ya vijijini, mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kwa wananchi na uelewa mdogo kuhusu masuala ya kijinsia hasa katika maeneo ya vijijini.

“Naomba niwakumbushe na maneno ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa kwanza mwanamke kuwahi kutokea katika Taifa hili aliyoyasema mwaka jana katika hafla kama hii. Nanukuu “Ningependa kuona usawa wa kijinsia wa 50/50, lakini si kwa ajili ya takwimu tu, bali kuhakikisha wanawake tunasonga mbele, tukiwa na uwezo wa kuleta mabadiliko” alisema.

Pia aliwahimiza wanawake kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi na kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu ambapo amesema ni muhimu kuona wanawake wakishiriki sio tu kama wapiga kura, bali kama wagombea, watetezi wa haki, na viongozi wa mabadiliko.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alihimiza utamaduni wa kusoma vitabu vinavyoeleza umuhimu wa kumkomboa mwanamke kwa malengo ya kuikomboa jamii dhidi ya misingi ya ubaguzi.

Akinukuu kitabu kilichoandikwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere zaidi ya miaka 80 iliyopita, Profesa Kabudi alisema mapambano dhidi ya ubaguzi wa kijinsi yameanza miaka mingi iliyopita na lengo lilikuwa ni kumkomboa mwanamke na kumwezesha kushika Madaraka na kushiriki nafasi za uongozi.

“Malengo ya Mwalimu Nyerere bila shaka yametekelezeka kwa kuwapata wanaweke viongozi na mfano halisi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan” alisema Profesa Kabudi.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema umefika wakati wa kurejea na kuondokana na mila mbaya zinazosababisha ukatili wa kijinsia.

Awali Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communication, Victor Mushi aliishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuunga mkono jitihada za kukuza vipaji na kuwaibua wanawake wenye mafanikio ikiwa ni njia mojawapo ya kuiwezesha jamii kuondokana na ukatili.
KAZI INAONGEA

No comments:

Powered by Blogger.