Richard Masele Achukua Fomu Kuwania Ubunge Itwangi
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com


Richard Raphael Masele
Na Kadama Malunde - Shinyanga
Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Richard Raphael Masele, leo Jumamosi Juni 28, 2025, ameibuka rasmi kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kwa kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chake kuwania nafasi ya Mbunge wa Jimbo jipya la Itwangi, mkoani Shinyanga.
Masele amesema amechukua hatua hiyo ya kuingia kwenye ulingo wa siasa za ubunge kwa lengo kuu la kuendeleza kazi kubwa ya maendeleo inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nimekuwa kiongozi wa CCM kwa zaidi ya miaka 20 katika nafasi mbalimbali. Nina uzoefu, dhamira, na maono ya kweli ya maendeleo. Nimeamua kugombea ubunge ili nimuunge mkono Mheshimiwa Rais Samia katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli,” amesema Masele.
Ameongeza kuwa atahakikisha anasimamia kwa vitendo utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kushirikiana na wananchi wa Itwangi, akiahidi kuwa chombo cha mabadiliko chanya ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Nitaendeleza yale mazuri yaliyofanywa na viongozi waliotangulia, hasa sasa ambapo Jimbo la Solwa limegawanywa na kuundwa kwa Jimbo la Itwangi. Huu ni wakati wa kuandika historia mpya,” amesisitiza Masele.
Jimbo la Itwangi ni mojawapo ya majimbo mapya yaliyoundwa kwa lengo la kuongeza uwakilishi wa karibu kwa wananchi na kurahisisha utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo.
No comments: