LIVE STREAM ADS

Header Ads

Hospitali ya Bugando yatoa elimu ya unyonyeshaji kwa akina mama

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Hospitali ya Kanda Bugando ya jijini Mwanza imetoa elimu kwa akina mama kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji maziwa ya mama ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama Duniani inayoadhimishwa kuanzia tarehe 01- 07 Agosti 2025.

Akizungumza Jumatano Agosti 06, 2025 wakati wa utoaji elimu hiyo, Daktari Bingwa wa Watoto Hospitali ya Bugando- Dkt. Florentina Mashuda amesema maziwa ya mama yana virutubisho kamili hivyo mzazi anapaswa kumnyonyesha mtoto maziwa pekee kwa miezi sita bila kumpa lishe yoyote ikiwemo maji.

Amesema baada ya miezi sita, mama anaweza kumuandalia mtoto chakula laini huku akiendelea kumnyonyesha kwa hadi atakapofikisha umri wa miaka kuanzia miaka miwili hadi mitatu kwa ukuaji wa afya ya mtoto kimwili na kiakili.

"Maziwa ya mama yana virutubisho vyote pamoja na kinga ya mwili ambayo inasaidia kumkinga mtoto na magonjwa mbalimbali ikiwemo nimonia na kuharisha" alisema Dkt. Mashuda.

Pia Dkt. Mashuda ameongeza kuwa kumnyonyesha mtoto kuna faida kwa akina mama ikiwemo kuepuka hatari ya kupata magonjwa ya saratani ya matiti pamoja na kusaidia kurudisha kizazi kwenye hali yake ya kawaida baada ya kujifungua.

Mmoja wa wazazi waliopata elimu hiyo, Happyness Samwel amesema yatawasaidia kuwalea vyema watoto wao hasa kuzingatia unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya awali na kwamba watafikisha elimu hiyo katika jamii inayowazungumza.

Kaulimu mbiu ya ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama duniani mwaka huu 2025 ni, "thamini unyonyeshaji: weka mazingira wezeshi kwa mama na mtoto".
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Daktari Bingwa wa Watoto Hospitali ya Bugando- Dkt. Florentina Mashuda akitoa elimu ya unyonyeshaji kwa akina mama waliojifungua hospitalini hapo.
Muuguzi Hospitali ya Kanda Bugando, Elia Woiso akizungumza na akina mama waliojifungua wakati wa utoaji elimu ya unyonyeshaji kwa akina mama hao.
Daktari Bingwa wa Watoto Hospitali ya Bugando- Dkt. Florentina Mashuda akitoa elimu ya unyonyeshaji maziwa ya mama kwa akina mama waliojifungua hospitalini hapo.
Picha ya pamoja baada ya elimu ya unyonyeshaji maziwa ya mama.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.