LIVE STREAM ADS

Header Ads

TADB YAFANYA SEMINA ELEKEZI KWA WANAHABARI KANDA YA ZIWA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendesha semina elekezi kwa waandishi wa habari kutoka Kanda ya Ziwa, ikiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano, kuongeza uelewa kuhusu majukumu ya benki, na kuonesha mchango wake katika kuendeleza minyororo ya thamani ya kilimo nchini.

Semina hiyo imefunguliwa Jumatano Disemba 03, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Saidi Mtanda, ambaye amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za kifedha na vyombo vya habari katika kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo.

Kupitia ufadhili wa miradi ya kimkakati, TADB inaendelea kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kusaidia uzalishaji wa mazao ya kibiashara, ufugaji wa kisasa, uvuvi na uchakataji wa mazao ya samaki. Benki pia inaweka mkazo katika kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika kilimo-biashara.

Hadi sasa, zaidi ya Shilingi bilioni 631 zimetolewa kufadhili miradi 151 katika Kanda ya Ziwa. Kati ya hizo, Mkoa wa Mwanza umepokea jumla ya Shilingi bilioni 79.14 kwa ajili ya miradi 61, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao, na kuchangia ukuaji wa uchumi wa wananchi.

TADB inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii, kuongeza uwazi, na kuhamasisha ushiriki mpana katika sekta ya kilimo.

Semina hii imehudhuriwa na zaidi ya waandishi wa habari 50 kutoka vyombo mbalimbali vya habari vinavyofanya kazi katika Kanda ya Ziwa.
#TADB #MediaDay #KandaYaZiwa #KilimoBiashara #Kilimokinabenkika

No comments:

Powered by Blogger.