LIVE STREAM ADS

Header Ads

SHIRIKA LA KIVULINI LAZINDUA MRADI WA KUTOKOMEZA UKEKETAJI TARIME

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la kutetea haki za wanawake la KIVULINI limezindua Mradi wa Kutokomeza Ukeketaji na Ndoa za Utotoni uitwao 'My Body, My Life', utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitatu kuanzia mwaka huu 2026 katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Shirika hilo lenye ofisi kuu jijini Mwanza linatekeleza mradi huo kwa upande wa Tanzania huku nchini Kenya ukitekelezwa na mashirika mawili ambayo ni KAKENYA'S DREAM na MICONTRAP kwa ufadhili wa shirika la FOKUS kutoka nchini Norway.

Uzinduzi huo umefanyika Ijumaa Februari 06, 2026 katika shule ya sekondari ya wasichana Borega wilayani Tarime ukiambatana na Madhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji yenye kaulimbiu isemayo, Sauti Yetu, Tokomeza Ukeketaji.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally alisema makundi mbalimbali ikiwemo mabinti walio shule na nje ya shule, waalimu, wazazi, maafisa maendeleo ya jamii, maafisa ustawi wa jamii, viongozi wa dawati la jinsia, viongozi wa Vijiji na Kata watajengewa uwezo na mbinu zitakazosaidia kutokomeza ukeketaji na ndoa za utotoni.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Siwema Sylivester alisema bado kuna changamoto ya vitendo vya ukeketaji kwa asilimia 28 katika Mkoa wa Maraa huku mbinu zinazotumika zikibadilika kutoka mbinu za wazi hadi za siri.

Alisema ili kukabiliana na ukeketaji na aina nyingine za ukatili wa kijinsia, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeunda Kamati za Ulinzi wa Mtoto katika ngazi za Kata ambazo zinasaidia kufichua matukio hayo na kuchukua hatua za kukabiliana nayo.

Wakizungumza wakati wa kongamano la Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukeketaji, baadhi ya mabinti wilayani Tarime walisema ukeketaji ni mila inayoweza kutokomezwa kupitia elimu. Walisema wazee huamini binti akikeketwa tayari anakuwa na sifa ya kuolewa na kuwapatia wazazi mali hivyo elimu ikiendelea kutolewa itasaidia kuondoa dhana hiyo.

Jamii za mpakani kati ya Tanzania na Kenya zimekuwa zikibadilishana mabinti kwa ajili ya ukeketaji hivyo mradi wa 'My Body, My Life' utasaidia kufikisha elimu kwa jamii hasa mabinti ili kutambua mapema madhara ya ukeketaji na kuchukua hatua ya kujilinda.

Ripoti zinaonyesha ukeketaji husababisha madhara mbalimbali yakiwemo ya kiafya, kihisia na kisaikolojia ambapo mhanga hupata maumivu makali, kutokwa damu nyingi, maambukizi ya maradhi, changamoto wakati wa kujifungua na hata kupoteza maisha.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Siwema Sylivester akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kutokomeza Ukeketaji na Ndoa za Utotoni (My Body, My Life) unaotekelezwa na Shirika la KIVULINI wilayani Tarime.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kutokomeza Ukeketaji na Ndoa za Utotoni (My Body, My Life) wilayani Tarime.
Mshauri wa Mradi kutoka Shirika la FOKUS la nchini Norway akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kutokomeza Ukeketaji na Ndoa za Utotoni (My Body, My Life) wilayani Tarime.
Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Jeshi la Polisi wilayani Tarime akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kutokomeza Ukeketaji na Ndoa za Utotoni (My Body, My Life).
Wanafunzi kutoka shule mbalimbali wilayani Tarime wakiwa kwenye uzinduzi wa Mpango wa Kutokomeza Ukeketaji na Ndoa za Utotoni (My Body, My Life) ulioambatana na Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji.

No comments:

Powered by Blogger.