CHAMA CHA WAGANGA NA TIBA ASILIA TANZANIA (CHAWATIATA) CHALAANI VIKALI MAUAJI YA ALBINO.
Na: George Binagi-GB Pazzo
Chama cha Waganga na Tiba Asilia Tanzania CHAWATIATA Mkoa wa
Mwanza Kimelaani na Kukemea vikali Mauaji ya Watu wenye Ulemavu wa ngozi ambayo
yameshamiri hapa nchini huku pia kikitoa onyo kali kwa waganga wa jadi
wanaochafua taaluma hiyo kwa kujihusisha na ramli chonganishi kujisalimisha
wenyewe polisi kabla hawajatiwa nguvuni.
Kauli hiyo ilitolewa jana Mkoani Mwanza yalipo Makao Makuu ya Chama hicho na
Kawawa Athuman ambae ni Katibu wa Chama hicho wakati akizungumza na Wanahabari
juu ya Kushamiri kwa vitendo vya Ukatili, Utekwaji na Mauaji kwa watu wenye
Ulemavu wa ngozi hapa nchini sanjari na Oparesheni ya Jeshi la Polisi
inayoendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwa na lengo la kuwasaka
waganga wa kienyeji wanaojihusisha na ramli chonganishi.
“Awali ya yote natoa tamko kwa niaba ya kamati ya CHAWATIATA Mkoa
wa Mwanza kulaani mauaji yote ya Albino yanayotendeka katika Mkoa wa Mwanza na
Tanzania nzima kwa ujumla na vilevile ninalaani wale wote wanaotumia kimvuli
cha Waganga wa Tiba Asilia kama wao ndio waganga”. Alisema Athuman huku
akiongeza kuwa,
“Hakika tiba asilia ni ni tiba ambayo ipo kihalali na kisheria
lakini kwa sababu tiba hii imevamiwa na wavamizi ambao si watu wanaitwa waganga,
tunaweza tukasema ni wavamizi wa waganga, hao ni majambazi wa waganga, hao ni
maharamia katika uganga huu, wanajihusisha na Mauaji ya Albino ambao wanakuja
kuchafua taasisi au taaluma ya watu ambao wamerithi miaka nenda rudi”. Alisema
Athuman huku akiwatahadharisha waganga wote wanaojihusisha na upigaji wa ramli chonganishi
kujisalimisha polisi kabla hawajatia nguvuni na jeshi hilo.
Nae Steve Sebastian ambae ni Katibu Mwenezi CHAWATIATA Mkoa wa
Mwanza aliitahadharisha jamii kuwa makini na baadhi ya watu wanaotumia
mazingaombwe huku wakijiita ni waganga kwa kuwa watu hao ni matapeli kwani wakiweka
matangazo mbalimbali kuonyesha kuwa wanatengeneza pesa jambo linachochochea mauaji
ya Watu wenye ulemavu wa ngozi ambapo aliodokeza kuwa CHAWATIATA imeanza
kuwabaini watu hao na inashirikiana na Serikali kiupitia jeshi la polisi kwa
ajili ya kuwakamata watu hao ambao wamekuwa wakijitangaza kuwa ni waganga.
Kwa upande wake Jumanne John ambae ni Mjumbe wa CHAWATIATA Wilaya
ya Nyamagana aliwaomba waganga wote kushirikiana kwa pamoja na Serikali kwa
lengo la kulaani mauaji ya Albino na Vikongwe huku akiongeza kuwa yeye hajui
Albino anatibu nini wala hajui ngozi ya mtu inatibu nini hivyo Ushirikiano wa
pamoja unahitajika kwa lengo la kukomesha mauaji ya Watu wenye ulemavu wa ngozi
pamoja na vikongwe hapa nchini.
Kauli
ya CHAWATIATA Mkoa wa Mwanza imekuja siku moja baada ya Jeshi la Polisi Mkoani
Mwanza kupitia kwa Kamanda Valentino Mlowola kueleza kuwatia nguvuni waganga 55
wakiwa na vitu mbalimbali ambavyo vinaaminika kutumika katika Shughuli za
Upigaji Ramli ambayo imepigwa marufuku na Serikali kutokana na kuleta
uchonganishi katika jamii ikiwa ni pamoja na kuongeza vitendo vya Ukatili,
Utekwaji na Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi hapa nchini hususani katika
Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Hamis Hassan ambae ni Mwenyekiti wa Chama cha Waganga na Tiba Asilia Tanzania CHAWATIATA akionyesha namna wanavyohifadi dawa za mitishamba kwa ajili ya tiba mbalimbali. |
No comments: