LIVE STREAM ADS

Header Ads

MATATA AWEKA BAYANA CHAMA ATAKACHOJIUNGA NACHO KATIKA UCHAGUZI WA MWAKA HUU.

Henry Matata
Na:George GB Pazzo
Diwani wa Kata ya Kitangiri Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza ambae pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Henry Matata ameweka bayana kuwa atatetea nafasi yake ya udiwani katika Kata hiyo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM, baada ya kutimuliwa ndani ya chama alichokuwa awali.

Matata aliingia madarakani Mwaka 2010 kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, lakini mwaka 2012 yeye pamoja na diwani wa Kata ya Igoma Adam Chagulani walitimuliwa ndani ya Chama hicho kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni usaliti ndani ya chama. Chagulani tayari nae ameweka bayana kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo.

Baada ya Kutimuliwa Matata pamoja na Chagulani walikimbilia Mahakamani na hivyo Mahakama kuweka zuio la kuvuliwa uanachama wao, na hivyo wakaendelea kushikilia nafasi zao za udiwani na hatimae mwaka 2012 Matata akachaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela baada ya Manispaa hiyo kugawanyika kutoka Halmashauri ya Jijini Mwanza.

Kutokana na hatua hiyo, Matata alibainisha kuwa katika Uchaguzi wa Mwaka huu anatarajia kutetea kiti chake cha Udiwani katika Kata ya Kitangiri kupitia Chama cha Mapinduzi CCM huku imani yake ikiwa ni kuchaguliwa kwa ushindi mnono kutokana na namna anavyowatumikia wananchi wake wa Kitangiri.

Matata alitoa kauli hiyo jana kupitia kipindi cha Chai Yetu kinachorushwa na Radio Saut ya Jijini Mwanza, ambapo alibainisha kwamba yeye kutimuliwa ndani ya Chadema haimuathiri kwa namna yoyote ile, kwa kuwa hata uchaguzi uliopita hakuchaguliwa na wanachadema pekee bali wananchi wa Vyama vyote hivyo hata akigombea kupitia CCM atachaguliwa na wananchi wa vyama vyote kwa kuwa wananchi hawaangalii vyama bali wanamchagua kiongozi anaewajibika kwa ajili ya maendeleo yao.
                             TAZAMA MATATA AKIWA KAZINI HAPA
                                        Credit:Radio Saut

No comments:

Powered by Blogger.