HALI MBAYA ILIYOPO BUGARIKA JIJINI MWANZA YAMLAZIMU MIRAJI MTATURU KUTOA AGIZO.
Na:George GB Pazzo
Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM
Mkoani Mwanza Miraji Mtaturu ametoa muda wa siku nne kwa Halmashauri ya Jiji la
Mwanza, kuhakikisha kwamba Uchafu uliozagaa katika dampo la Bugarika Sokoni
unaondolewa haraka iwezekanavyo.
Mtaturu
alitoa kauli hiyo jumamosi iliyopita alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Bugarika
Kata ya Pamba Wilayani Nyamagana katika Mkutano wa hadhara ikiwa ni katika kuadhimisha
Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Jumuiya ya Wazazi wa chama hicho Mkoani
Mwanza.
“Nimemwelekeza
Katibu wa Wilaya (Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana Elias Mpanda) amwambie
Mkurugenzi wa Jiji (Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Halifa Hida) ahakikishe
alhamisi sikuti takataka pale, nasema hivyo kwa sababu gani, zile takataka
zinazalisha maradhi kwa wananchi”. Alisema Mtaturu.
Aidha
alisema kuwa watendaji wa Serikali pamoja na viongozi wa kisiasa wanapaswa
kuwatumikia wananchi, na watakaoshindwa kufanya hivyo wanapaswa kuwajibishwa
ambapo katika hatua nyingine amewasihi wananchi kutowachagua viongozi wa
Kisiasa ambao hawawajibiki katika majukumu yao ambapo amemtolea mfano diwani wa
Kata ya Pamba Samwel Range (Chadema) kuwa nae ni miongoni mwa viongozi
wasiowajibika kwa ajili ya wananchini.
Mtaturu
alibainisha kuwa siku ya alhamisi wiki hii atafika katika damu hilo la Bugarika
Sokoni ili kujionea kama uchafu umeondolewa na akikuta bado uchafu huo
haujaondolewa basi viongozi wa eneo hilo ambao ni pamoja na Mtendaji wa Kata ya
Pamba wajiandae kuwajibika.
Pamoja na
kuwasihi wananchi wote kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la
Kudumu la wapiga kura wakati utakapofika, pia aliwahimiza Vijana kuacha
kulalamika kuwa hawawezeshwi badala yake wajiunge katika Vikundi ili kuweza
kutambulika na hivyo kufikiwa kirahisi kwa ajili ya kunufaika na fursa
zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya Vijana.
No comments: