HALI SI SHWARI JIJINI MWANZA. TAKWIMBU ZA WATUMIAJI WA DAWA ZA KULEVYA ZAONGEZEKA ZAIDI.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wanaopiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu nchini OJADACT Edwin Soko.
Na:George GB Pazzo
Idadi ya Watumiaji wa dawa za Kulevya Jijini
Mwanza imeelezwa kuongezeka hadi kufikia Watumiaji Elfu Kumi katika kipindi cha Miezi Minane
iliyopita, ikilinganishwa na idadi ya watumiaji Elfu Sita katika kipindi cha
mwaka jana.
Takwimu hizo ni kwa mjibu wa Mwenyekiti
wa Chama cha Waandishi wa Habari wanaopiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na
Uhalifu nchini (OJADACT) Edwin Soko, aliyoitoa jana wakati akizungumza na
Redio Metro juu ya Mchango wa Chama hicho katika kupambana na dawa za kulevya
nchini na zimelenga katika Wilaya za Nyamagana na Ilemela.
Soko alisema kuwa idadi hiyo
imeongezeka kutokana na kukosekana kwa njia mathubuti ya kupambana na
uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa hizo kutokana na wanaojihusisha na
biashara ya dawa hizo kubuni mbinu mpya za usafirishaji mara kwa mara jambo
linalosababisha ugumu katika kupambana na biashara hiyo.
Alifafanua usafirishaji na uingizaji
wa dawa za kulevya hapa nchini kwa njia ya Meli na ndege umepungua baada ya
njia hizo kudhibitiwa na polisi japo bado hatua hiyo haijazuia biashara ya dawa
za kulevya kufanyika kwa wasafirishaji wake wanatumia mbinu mbalimbali ikiwemo
kuambatanisha dawa hizo na bidhaa nyingine.
Alisema kuwa utumiaji wa dawa za
kulevya una athari kubwa ambazo ni pamoja na athari za Kiroho, Kimwili na
kiakili ambazo husababisha watumiaji kuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya
magonjwa mbalimbali ikiwemo virusi vya Ukimwi kwa wanaojidunga, kusababisha
uteja na hatimae kifo.
Hata hivyo Soko alibainisha kuwa
OJADACT inaendelea kutoa elimu dhidi ya mapambano ya dawa za kulevya kwa
kutumia mchango wa Waandishi wa Habari pamoja na kufikisha elimu hiyo kwa njia
ya midahalo na Sinema katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwemo Shule za
Msingi, Sekondari na Vyuoni.
Credit:Radio Metro
No comments: