LIVE STREAM ADS

Header Ads

MAONYESHO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI NANENANE MKOANI MWANZA, TFDA YATOA RAI KWA WANANCHI.

Judith Ferdinand
Jamii imetakiwa kushirikiana na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) katika kudhibiti na kupinga matumizi ya bidhaa zenye viambata vyenye sumu na zilizoisha muda wake wa matumizi.

Rai hiyo ilitolewa jana na Mkaguzi wa TFDA Kanda ya Ziwa Venance Buruph, wakati akizungumza na Binagi Media Group katika maonyesho ya Wakulima na Wafugaji Nane Nane yanayofanyika kwa Kanda ya Ziwa katika Viwanja vya Nyamongoro Jijini Mwanza.

Buruph alisema kuwa ili kukomesha matumizi ya vipodozi vyenye viambata vyenye sumu kwa watumiaji, jamii inatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuepuka matumizi ya vipodozi hivyo.

Pia alisema kuwa endapo kama suala hilo halitadhibitiwa mapema, litapelekea miaka ijayo kuwa na ongezeko la magonjwa mbalimbali ya ngozi ikiwemo Kansa ya ngozi, ini, figo pamoja na kuharibika kwa mfumo wa fahamu katika mwili wa mtumiaji.

"Pia mtumiaji wa vipodozi hivyo anaweza kushindwa kupata matibabu ikiwa atapata jeraha na wakati mwingine husababisha kidonda kuchelewa kupona au kutopona kabisa na hivyo kusababisha ulemavu. Alisema Buruph.

Kwa upande wake Mkaguzi  Mwandamizi wa Chakula TFDA Kanda ya Ziwa Julius Panga, alisema kuwa uuzaji wa bidhaa ambazo  zimefika kikomo cha matumizi ni uzembe wa muuzaji na aliwasihi wafanyabiasha kujijengea utaratibu wa kukagua bidhaa zao kila mara ili kubaini mwisho wa matumizi yake.

Pia aliwaomba wananchi kufuatilia bidhaa wanazonunua ili kujua kama zimekwisha muda wa matumizi yake pamoja na kutoa taarifa kwa TFDA pindi wanapobaini madukani kuna bidhaa wanazozitilia mashaka.

Maonyesho hayo ya Nane Nane yalianza juzi jumamosi Agosti Mosi na yanatarajiwa kufikia tamati jumamosi ijayo ya Agost nane na wananchi wamehimizwa kufika kwa wingi katika maonyesho hayo ili kujionea bidhaa mbalimbali zilizopo kutoka Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa.

No comments:

Powered by Blogger.