LIVE STREAM ADS

Header Ads

SERIKALI YAOMBWA KUINGILIA KATI MGOGORO WA KISIASA KATIKA KATA YA BUGARAMA WILAYANI KAHAMA.

Na:Shaban Njia
Serikali katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga, imeombwa kuingilia kati marumbano ya kisiasa baina ya Wagombea wawili mmoja kutoka Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA na mwingine wa Chama cha Mapinduzi CCM waliokuwa wakigombea Udiwani katika Kata ya Bugarama kutokana na kukitishiana maisha baada ya mmoja wao kutangazwa.

Wagombea hao ambao ni Joseph Izengo CHADEMA na Prisca Msoma CCM, wamekuwa na mgogoro wa chini kwa chini hali ambayo imezua taharuki kubwa kwa wananchi wa Kata hiyo.

Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti, Wagombea hao kila mmoja alimtupia lawama mwenzake huku mgombea aliyeshinda kwa tiketi ya Chadema Joseph Izengo akisema kuwa yeye ameshinda kiuhalali na alitangazwa kuwa mshindi na msimamizi  wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria.

Izengo alisema kuwa baada ya mgombeakwa tiketi ya CCM kulalamika kuwa ameibiwa kura na kulazimisha maboksi yote yarudiwe, msimamizi aliamuru maboksi mawili ya kura yahesabiwe upya jambo ambalo lilitekelezwa lakini mgombea huyo bado hakuwa na imani nayo na kuamuru yarudiwe yote ambapo msimamizi aligoma hali iliyosababisha mgombea huyo kukataa kusaini matokeo.

“Mimi ndiye mshindi wa Udiwani kata ya Bugarama hakuna Diwani mwingine, nimetangazwa na msimamizi wa uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, hakuna kura zilizoibiwa na nimepokea barua yenye vitisho na sijajiandikia mwenyewe kujitisha. Wameniandikia barua ya vitisho na kuitupa nyumbani kwangu ikiwa inaeleza kuwa niachie kata hii kwani haiwezi kuongozwa na upinzani. Alisema Izengo na kuongeza kuwa barua hiyo pia ilikuwa imechorwa mapanga na viashiria vingine vya vitisho.

Kwa upande wake aliyekuwa mgombea Udiwani kwa tiketi ya CCM katika kata hiyo Prisca Msoma, alisema kuwa yeye hajahusika na kuandika barua hiyo na baada ya kumaliza Uchaguzi aliondoka kwenda Bukombe Geita kusalimia ndugu yake huku akitafakari jinsi Uchaguzi huo ulivyomalizika na kuongeza kuwa kura alizoshinda mgombea huyo si za halali bali ni ziliibiwa kutoka kwake.

“Baada ya Uchaguzi niliondoka nikaenda Wilaya ya Bukombe kusalimia ndugu yangu wakati huo nikitafakari jinsi ya kufungua kesi, kwani mshindi nilikuwa mimi. Nilikataa kusaini kwa kuwa nililazimishwa kuwa nimeshindwa. Hapa najiandaa kufungua kesi ya kupinga matokeo hayo”. Alisema Msoma.

No comments:

Powered by Blogger.