CCM KUONGOZA BARAZA LA MADIWANI KATIKA MANISPAA YA ILEMELA MKOANI MWANZA.
Judith Ferdinand, mwanza
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza, jana limefanya uchaguzi wa Meya na Naibu Meya ambapo Chama cha Mapinduzi CCM kimeibuka na ushindi katika nafasi hizo.
Naibu Meya aliyeshinda ni Shambani Maganga(CCM) diwani wa kata ya Nyasaka kwa kura 21 dhidi ya John Nyemhanga wa Kata ya Kitangiri (CHADEMA) aliyepara kura nne ambapo kura zilizoharibika zilikuwa ni mbili huku jumla ya kura zilizopigwa zikiwa ni 27.
Meya wa halmashauri ya Manispaa ya ilemela ni Renatus Mulunga kutoka Kata ya Sangabuye (CCM) ambae alipata kura 22 dhidi ya Abubakary Kapera wa kata ya Nyamanoro (Chadema) aliepata kura nne, kura moja iliharibika ambapo jumla ya kura zilizo pigwa zilikuwa ni 27.
Baada ya kuchaguliwa, Meya Mulunga alisema atahakikisha halmashauri hiyo inapata miundombinu kama barabara na katika elimu wanafunzi wanapata elimu bora kwa kuwezesha vitendea kazi ikiwemo madawati na vitabu pamoja na kuwajengea walimu nyumba kupitia mapato yanayokusanywa na halmashauri ili kuhakikisha hawatembei umbali mrefu kwenda kazini.
Alisema atasimamia suala la ardhi kwa kutoruhusu upimaji wa viwanja ufanyike kabla vikao vya baraza la madiwani halijakaa na kujiridhisha pamoja na kushirikisha wananchi ili kuepusha migogoro ya ardhi.
Pia alisema waliopewa tenda ya kukusanya mapato ya halmashauri wakienda kinyume na masharti kwa kutokusanya ushuru na kodi walizopangiwa watakuwa wamevunja mkataba.
Hata hivyo alisema, atahakikisha anasimamia vyema baraza hilo ili kila diwani awajibike ipasavyo ili wananchi wapate haki zao maana hatakubali kuacha mianya ya watendaji wabovu ili kuendana na kasi ya Rais ya HAPA KAZI TU.
Naibu meya Maganga alisema, Atahakikisha anashirikiana na Meya ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa ilemela na kwamba atatekeleza ahadi zake zote alizowaahidi wananchi wa kata ya Nyansaka wakati akiwaomba kura.
No comments: